1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yawatimua wanasiasa 19 kwa makosa ya usaliti

Florence Majani12 Mei 2022

Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nchini Tanzania limeunga mkono maamuzi ya kamati kuu ya chama hicho ya kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa viti maalum.

Tansania | Chadema | Entlassung von Abgeordneten | in  Dar es Salaam
Picha: Eric Boniphace/DW

Wabunge hao, wote wanawake, walikubali uteuzi ambao chama chao kilisema haukukihusisha. 

Ilikuwa ni saa saba na dakika 34  za usiku, ambapo Baraza Kuu la chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania lilihitimisha mchakato wa  kuwapigia kura na kuwahoji wabunge 19 wa Viti Maalum na hatimaye kuja na uamuzi  wa kuwavua uanachama.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu umefanyika kwa kupiga kura huku ukishuhudiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Syst Nyahoza.

Mchakato wa upigaji kura, ulihusisha wapiga kura  423, ambapo wajumbe wasiounga upande wowote walikuwa watano na kura za hapana zilikuwa tano  huku wajumbe waliokubaliana na  maamuzi ya kamati kuu wakiwa  ni 413.

Hivyo  basi, kwa matokeo hayo yaliyotolewa na Mkuu wa Mawasiliano wa Chadema  John Mrema, ni dhahiri kwamba, wabunge hao 19 wamevuliwa uanachama.

Soma pia: Rais Samia: Tanzania haiwezi kujengwa na chama kimoja

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Aikaeli Mbowe amesema, "Tumesikitioa na hatujafurahia hali hiyo. Lakini imebidi. Maamuzi ya kuwafukuza yamefanyika tangu mwaka juzi kwenye kikao cha Kamati Kuu. Tangu mwaka juzi hatujakaa kikao cha Baraza Kuu, Baraza Kuu limekaa leo na wao walikuwa ni mashuhuda na wameona maamuzi ya wajumbe. Sasa wakilalamika maamuzi yalifanyika kabla. Yalifanyika wapi na wajumbe walikuwa wapi? Wajumbe wamekuja leo na maamuzi yamefanyika leo na kura zimepigwa mbele yao. Waache mambo ya kihuni."

Halima Mdee: Kilichotokea ni uhuni wa kiwango cha hatari.

Aliyekuwa mwanachama wa Chadema Halima Mdee akizungumza na wanahabariPicha: Eric Boniphace/DW

Mchakato wa kupitia barua zao za rufaa  ulianza saa  4:28 usiku, na ilipofika saa TANO usiku, waliitwa mmoja mmoja kwa ajili ya kuhojiwa na kisha upigaji kura ulianza.

Hata hivyo maamuzi yaliyofikiwa mnamo saa 7:34 usiku yalikuwa ni kuwavua uanachama.

Akizungumzia uamuzi huo, Mbunge wa Viti Maalum, aliyevuliwa uanachama, Halima Mdee amesema, "Kwa ufupi ni kwamba nadhani mlikiwa mnasikiliza kilichoendelea pale si upigaji kura, kwa wapigw kura kuwa huru. Ila kilichotokea pale unaweza kusema ni uhuni. Unajua nimekuwa kimya muda mrefu. Nitaongea siku nyingine leo si wakati muafaka. Lakini sikujua kama Chadema kunaweza kufanyika uhuni wa kiwango hicho. Mimi ni Chadema na nitaendelea kuwa Chadema lakini kilichofanyika pale 'My Friend' ni uhuni wa kiwango cha hatari."

Utata wa nafasi za kibunge za wabunge hawa ulianza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 huku Chadema kikishikilia msimamo wa kutokubaliana na matokeo hayo yaliyompa ushindi Hayati John Magufuli.

Soma pia:Kiongozi wa upinzani Tanzania aachiwa huru 

Kwa kuwa chadema hakikutambua matokeo hayo, hakikuafiki wabunge 19 wa Viti Maalum kuingia bungeni  hata hivyo, Wabunge hao waliendelea kuhudhuria bunge  hadi pale Kamati Kuu ilipowavua uanachama.

Baadaye walikata rufaa  katika Baraza Kuu la chama hicho, wakipinga uamuzi huo na leo Baraza hilo, limehitimisha kuwaondoa.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John John Mnyika, amesema anatarajia kupeleka barua rasmi kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, ili kumtaarifu kuhusu uamuzi huo.