1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yazinduwa 'Operesheni 255' kudai katiba mpya

17 Mei 2023

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimezindua hivi leo kampeni maalumu ya kudai katiba mpya ikiwa ni takribani wiki mbili tangu Rais Samia Suluhu wa nchi hiyo kutangaza azma ya kuufufuam mchakato huo.

Tansania | Opposition | Feier zum internationalen Frauentag
Picha: Emmanuel Ntobi

Uzinduzi huo umefanywa na viongozi wote wa chama hicho ngazi ya taifa, kanda na mkoa wa Kigoma katika viwanja vya Mwanga mjini Kigoma, ambapo mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisisitiza kuwa "Tanzania inahitaji katiba mpya."

Moja ya mambo yanayotajwa kusukuma madai ya katiba ni kuzorota kwa huduma za jamii, wananchi kunyimwa haki, wanawake kukandamizwa na sheria kuwepo kwa zinazoumiza wananchi, hasa kwenye kodi na ushuru wa biashara.

Soma zaidi: Rais Samia aungana na Chadema kuadhimisha siku ya wanawake

Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la chama hicho, Catherine Ruge, ambaye kabla ya mkutano huo alilitembelea soko maarufu kwa wanawake wajasiriamali, Nazareth la mjini Kigoma, alisema ni dhahiri kuwa wanawake hao wajasirimali hawataweza kujikwamua ikiwa katiba ya sasa itaendelea kuwapo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho kwa mkoa wa Kigoma, Boniphace Chuzura, alisema "serikali ya CCM  imeshindwa kushughulikia matatizo ya kaya masikini kupitia mradi wake TASAF kwa kuwatumikisha kutengeneza barabara za mitaa", kazi ambayo yeye alisema inapaswa kufanywa na Mamlaka ya Barabara (TARURA).

Muundo wa Muungano wakosolewa

Wanachama wa CHADEMA katika moja ya mikutano yao nchini Tanzania.Picha: Emmanuel Ntobi

Kuhusu suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema ingawa Muungano huo una faida lakini pia unazo kasoro nyingi, ikiwemo ya "kutokuwepo na serikali ya Tanganyika. 

Soma zaidi: Tanzania: CHADEMA yaanza kupokea ruzuku ya serikali

Ingawa kuanza kwa mchakato huu kunahusishwa moja kwa moja na nia ya Rais Samia Suluhu kuirejesha nchi kwenye utaratibu wa kidemokrasia kufuatia miaka sita ya mtangulizi wake, Marehemu John Magufuli, iliyowacha makovu mengi nchini huko, lakini Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema ana mashaka na mwelekeo wa serikali kuonesha nia ya kufufua mchakato wa katiba mpya, akihoji kuhusu bajeti na mabadiliko ya sheria.

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa maeneo yaliyowahi kuwa ngome ya CHADEMA kabla ya mvuto wake kupotea na kuchukuliwa na ACT wazalendo na baadaye CCM kutwaa majimbo yote na kata zote katika uchaguzi wa maka 2020.