1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chaguzi za mchujo Marekani zaanza kwa mashaka

4 Februari 2020

Chaguzi za mchujo zimeanza kumsaka mgombea urais wa Democrat atakayepambana na Donald Trump wa Marekani kwenye uchaguzi wa Novemba 2020, lakini mashaka yamezuka jimboni Iowa, baada ya mfumo wa kielektroniki kukwama.

USA Vorwahl der US-Demokraten in Iowa
Picha: picture-alliance/ZumaPress/S. Dorfman

Katika uchaguzi huu wa kwanza wa mchujo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba, matatizo kwenye programu maalum ya simu ya mkononi kwa ajili ya upigaji kura yalisababisha kuchelewa kutangazwa kwa matokeo jimboni Iowa siku ya Jumatatu (3 Februari).

Hadi asubuhi ya Jumanne, timu za kampeni, wapiga kura na vyombo vya habari vilikuwa havijamjuwa mshindi, huku watu wakitaka majibu na maelezo ya haraka. 

Chama cha Democrat kwenye jimbo hilo kilitangaza kuwa matokeo yangelitolewa siku ya Jumanne (4 Februari), baada ya kuhisabu na kupitia kura kwa mikono, huku mwenyekiti wa chama hicho Troy Prince akisema ucheleweshwaji wa matokeo umetokana na tatizo la kuripoti na wala sio kudukuliwa kwa mfumo wa kura kama wengine walivyodhani.

"Heshima ya mchakato wetu na matokeo yake daima limekuwa jambo la kipaumbele chetu. Ndio maana tuna mifumo ya kunakili kura kwenye karatasi ili kudumisha heshima ya mchakato wetu. Maafisa wetu wanapitia kila kura na kuthibitisha kwenye fomu zetu."

Lakini waandaaji wengine wa chaguzi hizi za mchujo walisema kuwa teknolojia mpya inayotumika kwenye chaguzi 1,700 kwenye jimbo hilo hauko sawa. Baadhi yao walilazimika kuitisha matokeo ya kura kwa kwenye karatasi ili kuthibitisha.

Bernie Sanders adai kushinda

Wafuasi wa Barnie Sanders walidai mgombea wao alishinda Iowa.Picha: Getty Images/R. Beck

Seneta Bernie Sanders alidai kushinda kwenye uchaguzi huo wa mchujo akirejelea matokeo yaliyokusanywa na timu yake ya kampeni, akimshinda Pete Buttigieg.

Matokeo yaliyotolewa usiku wa Jumatatu na timu yake yakihusisha asilimia 40 ya kura yalimuonesha Sanders akiongoza kwa asilimia 28.6 mbele ya Buttigieg mwenye asilimia 25.7. "Usiku huu ni muhimu sana kwa uchaguzi wa 2020, jimbo la kwanza nchini limepiga kura leo, na leo ni mwanzo wa mwisho wa Donald Trump," alisema Sanders mbele ya wafuasi wake.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya timu ya Sanders, wapinzani wake wengine walikuwa nyuma yake sana, ambapo Seneta Elizabeth Warren alikuwa na asilimia 18 akishika nafasi ya tatu na makamu wa rais wa zamani, Joe Biden, akishika nafasi ya nne kwa kupata asilimia 15.

Hata hivyo, matokeo haya ya timu ya Sanders hayawezi kuthibitishwa hadi hapo matokeo rasmi yatakapotolewa na chama chake cha Democrat. 

Ingawa jimbo hilo la magharibi lina idadi ndogo ya wapigakura, kihistoria linachukuliwa kuwa muhimu kwani ndilo ambalo huchochea pakubwa nafasi ya mshindi wa kitaifa.

Lakini tatizo hili lililojitokeza huenda likaathiri sifa yake hiyo ya kihistoria na pia kubadilisha mtazamo wa wapigakura kwa chama hicho cha Democrat.