Chakwera akubali kushindwa na mpinzani wake
24 Septemba 2025
Baada ya kupata taarifa kwamba mpinzani wake alikuwa anaongoza kwa zaidi ya kura asilimia 60 zilizohesabiwa, Rais Chikwera ametoa tamko kwamba amekwisha kumpigia simu Mutharika na kumpongeza kwa ushindi.
"Wenzangu raia wa Malawi, siku mbili zilizopita tume ya uchaguzi ilitangaza matokeo yaliyothibitishwa kutoka mabaraza 11 na kufikia 24 na kutokana na matokeo hayo rasmi, ni wazi kwamba mpinzani wangu, Profesa Peter Mutharika wa chama cha DPP, tayari amepata kuongoza pakubwa na kwa hiyo ndiyo mshindi anayebashirika katika uchaguzi wa urais."
Awali Chakwera alikuwa amewasilisha shauri katika Mahakama Kuu akipinga matokeo kwa madai kuwa palitokea udanganyifu. Lakini hapo jana, Mahakama hiyo ililitupilia mbali shauri hilo ikisema kuwa madai yake hayakuwa na msingi wowote.
Kabla ya uchaguzi huo uliofanyika wiki iliyopita, wagombea wawili hao - Chakwera mwenye umri wa miaka 70 na Mutharika mwenye umri wa miaka 85 - ndio waliobainika kuwa na mvuto mkubwa kuliko wagombea wenzao 15 kwenye kiti cha urais.
Katika kampeni zake, Mutharika wa chama cha DPP alitumia kauli mbiu ya kurejelea uongozi uliothibitika kuleta maendeleo ya kiuchumi katika nchi hiyo inayorodheshwa kuwa miongoni mwa mataifa masikini kabisa barani Afrika.
Kulingana na wapiga kura, suala la mfumko wa bei za bidhaa muhimu ikiwemo chakula, mafuta na mbolea lilikuwa nyeti katika kuongoza maamuzi ya nani wamchague safari hii.
Rais Chakwera wa chama cha MCP amekosolewa vikali kwa kuzorotesha uchumi wa nchi na kusababisha hali ngumu ya maisha hasa kiutokana na kushindwa kufanya maamuzi stahiki na wakati muafaka. Licha ya umasikini wake, taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika limekuwa na historia ya aina yake ya ubalishanaji madaraka kwa njia ya chaguzi za kidemokrasia.
Itakumbukwa kuwa Chakwera alimshinda Mutharika katika uchauguzi uliorudiwa mwaka 2020 baada ya matokeo yake kufutiliwa mbali na mahakama kwa msingi kwamba zoezi hilo liligubikwa na mapungufu mengi. Hii ilikuwa baada ya nchi hiyo kushuhudia ghasia kufuatia uchaguzi wa mwaka 2019.
Kakake Mutharika, Bingu wa Mutharika, alitawala nchi hiyo kati ya mwaka 2004 hadi 2012 alipofariki akiwa madarakani. Rais Chakwera amelezea kuwa katika siku zilizobaki za utawala wake atapanga kukabidhisha madaraka kwa amani.