ACT-Wazalendo chazindua ilani ya uchaguzi, Zanzibar
8 Oktoba 2025
Muda mfupi baada ya kuzindua ilani hiyo kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip kando kidogo mwa kitovu cha Mji wa Unguja, mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema ilani yao hiyo imejikita kwenye misingi minne mikuu ya kile alichokiita "Kuinusuru Zanzibar" ambayo ni uchumi, mamlaka kamili, upatikaji wa haki na masuala ya kijamii, lakini akitilia umuhimu zaidi suala la haki za Zanzibar kwenye Muungano.
"Tunachukulia Muungano kama eneo la haki na siyo fadhila. Zanzibar, kama mshirika kamili, inastahili Mamlaka Kamili na Heshima inayostahiki," alisisitiza.
Aidha ameahidi kurejesha utengemano wa kijamii kupitia maridhiano ya kweli na kuongoza mageuzi katika maadili na malezi, "Kwa miaka mingi, Zanzibar imekabiliwa na changamoto zinazojirudia na zinazohatarisha maisha yetu.
Aliongeza kuwa "Ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Huduma duni za afya na mfumo wa elimu unaoporomoka. Utawala wa kibabe usiozingatia maslahi ya wengi. Na la hatari zaidi, kukosekana kwa utii wa sheria na kufeli kwa mfumo mzima wa kutoa haki."
Kuzinduliwa ilani hiyo kunakwenda sambamba na mikutano ya kampeni ambapo mbali na kunadi sera zake, chama hicho kimekuwa kikiibuwa kashfa mbalimbali kinachosema ni ufisadi uliotendwa na uongozi wa miaka mitano wa CCM.