1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha AfD chataka kuitawala Ujerumani

Josephat Charo
6 Julai 2026

Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD kimethibitisha tena nia yake ya kutaka kuitawala Ujerumani. Kauli hii imetolewa na kiongozi mwenza wa chama Alice Weidel katika mkutano mkuu wa chama uliokamilika jana mjini Erfurth.

Deutschland Erfurt 2026 | AfD-Parteitag | Alice Weidel & Tino Chrupalla auf der Bühne
Picha: Karina Hessland/REUTERS

Akihitimisha mkutano mkuu wa kitaifa wa chama hicho huko Erfurt, mji mkuu wa jimbo la mashariki la Thuringia, kiongozi mwenza aliyechaguliwa tena Alice Weidel amesema chama kiko tayari kutawala baada ya kupata mafanikio makubwa katika kura za maoni.

Weidel alikuwa akizungumzia kura za maoni za sasa ambazo zinaonyesha chama hicho kikiongoza kote Ujerumani. Alisema "Sisi ndio nguvu kubwa zaidi. Sisi ni chama cha watu chenye uungwaji mkono wa asilimia 30. Na tutatawala".

"Tuna lengo moja, nalo ni Ujerumani. Lengo hilo ni jeusi, jekundu na la dhahabu, rangi za bendera yetu. Tunataka kuirudisha nchi yetu na ya baba zetu kwenye njia sahihi. Tunalenga kikamilifu uchaguzi ujao wa majimbo mwezi Septemba huko Saxony-Anhalt na Mecklenburg-Western Pomerania ambapo tutatoa mawaziri wakuu wa majimbo, marafiki wapendwa, na huko Berlin."

Chama cha AfD pia kilijadili misimamo ya ndani na mabadiliko ya kanuni zake za kudumu, kuhusu kusajili wanachama wapya na ada za chama.

Alice Weidel na Tino Chrupalla walithibitishwa kuwa viongozi wenza, huku baadhi ya nafasi katika kamati kuu ya utendaji wa chama zikijazwa na wanachama 14 waliochaguliwa kama wagombea wapya.

Alice Weidel, kulia, na Tino Chrupalla wamechaguliwa kama viongozi wenza wa chama cha AfDPicha: Karina Hessland/REUTERS

Mkutano wa chama cha AfD ulihitimishwa katika jiji la mashariki la Erfurt siku ya Jumapili huku chama hicho kikijadili masuala ya ndani na mamlaka za jiji zikihesabu gharama ya maandamano makubwa ya kukipinga chama hicho.

Katika ukumbi wa mikutano maafisa wa chama waliwasilisha video kuhusu uchaguzi ujao wa majimbo katika majimbo ya mashariki ya Saxony-Anhalt, Mecklenburg-Vorpommern na jiji la Berlin.

Chama cha AfD kinalenga kupata wingi kamili wa viti katika jimbo la Saxony-Anhalt, ambapo kura za maoni zinaonyesha kina asilimia karibu 41. Kura zilizopotea zinaweza kusukuma hilo hadi zaidi ya asilimia 50 ya viti katika bunge la jimbo na kukipa chama udhibiti katika ngazi ya jimbo kwa mara ya kwanza.

Pistorius aonya kuhusu AfD kuongoza serikali ya jimbo

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ameelezea wasiwasi wake kuhusu chama hicho kuwa sehemu ya serikali ya jimbo, akirejelea msimamo wa AfD kuhusu rais wa Urusi Vladimir Putin katika mahojiano na toleo la Jumapili la gazeti la Bild linalosambazwa kwa wingi.

Pistorius alisema na hapa tunanukuu "Ukaribu wao na Putin hauwezi kupuuzwa. Tuhuma kwamba kuna fedha kutoka Urusi pia zimetolewa," Pistorius aliongeza kuwa taarifa nyeti hazipaswi kuruhusiwa kupita mikononi mwa watu wasiofaa.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ameonya kuhusu chama cha AfD kuunda serikali ya jimboPicha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Pistorius alisema Jumapili kwamba serikali ya shirikisho inazingatia kuzuia taarifa kutoka kwa mawaziri katika tawala za majimbo ikiwa zitaundwa na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani AfD.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa chama cha AfD kinaweza kushinda kura nyingi katika uchaguzi wa majimbo mwezi Septemba huko Saxony-Anhalt, kumaanisha kwamba kitaunda serikali ya jimbo kwa mara ya kwanza.

Chini ya mfumo wa shirikisho wa Ujerumani, serikali za majimbo zina mamlaka makubwa katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na shughuli za polisi na huduma za ujasusi.

Alipoulizwa na gazeti la Bild kama serikali ya jimbo ya AfD ingekuwa na athari kwa kambi za jeshi katika majimbo hayo, Pistorius alisema: "Tunaangalia kwa makini sana suali la ni nani tunayeweza kuruhusu ufikiaji wa taarifa za siri. "Tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu inahusu usalama wa nchi yetu."

Pistorius, ambaye ni wa chama cha Social Democratic SPD cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto, alisema angehisi wasiwasi kusambaza taarifa zilizofichwa kwa waziri wa jimbo wa chama cha AfD.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW