Chama cha AKP kimeshinda uchaguzi Uturuki
23 Julai 2007Chama cha kihafidhina cha AKP cha Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan,kilitazamiwa kushinda uchaguzi wa bunge,lakini ni wachache sana walioamini kuwa kitaweza kushinda kwa uwingi kama huo.
Kwani baada ya takriban kura zote zilizopigwa kuhesabiwa Jumapili jioni,ilidhihirika kuwa chama cha AKP kimeshinda kwa asilimia 47,hiyo ikiwa ni zaidi ya asilimia 12 kulinganishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2002.Lakini kwa sababu ya muungano wa vyama vya upinzani,AKP kitakuwa na viti 340 katika bunge la viti 550.Hata hivyo chama AKP chenye mizizi ya siasa za Kiislamu sasa kimepata viti vya kutosha bungeni,ili kuweza kuunda serikali ya chama kimoja.
Mbali na chama cha AKP,hata vyama vya CHP na MHP vile vile vimefanikiwa kuingia bungeni baada ya kuvuka kiwango cha asilimia 10 kinachohitajiwa.Lakini matokeo hayo ni kinyume ni vile vyama hivyo viwili vilivyotazamia kushinda. Mbali na vyama hivyo vitatu,wagombea wengine 25 wa kijitegemea wamefanikiwa pia kuingia bungeni. Wengi wao ama ni wanachama au wajumbe wanaokiounga mkono chama cha DTP ambacho huwaunga mkono Wakurdi.
Kwa upande mwingine,waziri Mkuu Erdogan alipojitokeza mbele ya umma uliokuwa ukishangiria ushindi wa chama cha AKP alisema:
„Ushindi wa uchaguzi huu wa bunge ni ushindi wa umma,mustakabali wetu pamoja na utulivu wa nchi.“
Akaongezea kueleza kuwa serikali yake itaendelea na jitahada zake ili Uturuki iweze kupokewa kama mwanachama kamili katika Umoja wa Ulaya. Amesema,hata mageuzi ya kidemokrasia yatakwenda kwa kasi kubwa.
Inasemekana kuwa ni mambo mawili yaliyochangia ushindi wa Erdogan.Kwanza,ni hali nzuri ya uchumi iliyopo hivi sasa nchini Uturuki.Kwani uchumi wa Uturuki umekuwa kati ya asilimia 6 hadi 9 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Pili,ni hamaki ya umma,iliyosababishwa na jeshi la Uturuki.Waziri Mkuu Erdogan alipomteua waziri wake wa nje,Abdullah Gul kugombea wadhifa wa urais,hatua ambayo ilipingwa na kushindwa,jeshi lilitishia kuipindua serikali.Lakini Gul alie muumini wa Kiislamu sawa na Erdogan,hivi sasa ni mwanasiasa anaependwa kuliko wote nchini Uturuki.Kwa maoni ya Hassan Cemal,mhariri wa gazeti la kiliberali la Kituruki “Milliyet“ matokeo ya uchaguzi wa siku ya Jumapili ni barua ya umma kwa matamshi ya jeshi.
Ushindi wa chama cha AKP cha Waziri Mkuu Erdogan, umekaribishwa pia na Umoja wa Ulaya.Hii leo umoja huo umetoa wito kwa Erdogan kuendelea na mageuzi yaliyokwama.Mageuzi hayo yanahitaji kutekelezwa kwani yanafungamana na uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya.