1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ANC chagawika kuhusu uchunguzi wa rushwa

2 Mei 2021

Rais Cyril Ramaphosa anasema chama tawala cha Afrika Kusini ANC kilipaswa kufanya zaidi kupambana na rushwa wakati wa muhula wa Jacob Zuma. Alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ya rushwa inayohusu familia ya kina Gupta.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Reuters/R. Bosch

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alijitokeza mbele ya tume ya uchunguzi mjini Johannesburg kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ngazi ya juu kuhusu rushwa wakati wa muhula wa miaka tisa ya rais wa zamani Jacob Zuma. Uchunguzi huo unahusisha tuhuma kwamba Zuma aliwaruhusu wafanyabiashara ndugu Atul, Ajay na Rajeshi Gupta, kushawishi sera zake na kushinda zabuni nono za serikali, jambo lililosabisha maandamano ya nchi nzima mwaka 2017, dhidi ya kile wengi walikieleza kama "utekaji wa serikali."

Ramaphosa alisema makada wa juu wa chama tawala cha African National Congress ANC walitofautiana na iwapo kundi dogo la watu lilikuwa na ushawishi usiostahiki juu ya serikali. "Tofuati juu ya iwapo kweli kulikuwepo na utekaji wa serikali, ukubwa wake na muundo, na nini kinapaswa kufanyika juu yake zilichangia kwenye migawanyiko ndani ya kamati ya taifa ya utendaji na miundo mingine ya ANC," Ramaphosa aliiambia tume.

Soma pia: Zuma asema hana hatia katika tuhuma za rushwa

Rais huyo pia alihojiwa kuhusu kamati ya uwekaji wa makada wa ANC. Kamati hiyo ina jukumu la kuwaweka wanachama katika nyadhifa muhimu serikalini. Tume ilibainisha baadhi ya nafasi nyeti serikali kama chanzo cha  vitendo endelevu na visivyodhibitiwa vya rushwa ndani ya serikali.

Waandamanaji wakiwa na mabango yanayopinga kile kilichoitwa "utekaji wa serikali" na wafanyabiashara ndugu kina Gupta kutokana na ushawishi wao ndani ya serikali.Picha: Getty Images/AFP/A. Debiky

Ramaphosa alikiri kwamba kamati hiyo iliruhusu kuwekwa kwa wanachama wasio na uwezo katika baadhi ya nafasi muhimu lakini alitetea uamuzi huo kama muhimu kutimiza mamlaka ya chama.

ANC yakiri makosa

Rais alikuwa akijibu maswali kama mkuu wa chama cha ANC. Alisema chama hicho tawala "kingeweza na kilipaswa" kufanya zaidi ili kuzuwia rushwa chini ya mtangulizi wake Zuma.

"ANC inakiri ilifanya makosa," Ramaphosa alisema. "Ilikuwa na kasoro katika kutimiza matarajio ya watu wa Afrika Kusini kuhusiano na kutekeleza uwajibikaji," aliongeza.

Kutokea kwa Ramaphosa kuliashiria mara ya kwana ambapo rais alieko madarakani alitoa ushahidi dhidi ya mwanachama wa chama chake.

Rais aliiambia tume kwamba ANC ilisubiri muda mrefu sana kutambua rushwa iliyokithiri wakati wa kipindi hicho lakini kwmaba hatojaribu kutoa "visingizio au kutetea wasiowezekana kutetewa." Ramaphosa hakumtaja bosi wake wa zamani, Zuma, kwa jina.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiwa amekaa karibu na aliekuwa makamu wake Cyril Ramaphosa, ambaye ndiye rais wa sasa wa taifa hilo.Picha: Reuters/S. Sibeko

Waafrika Kusini wengi walimsifu Ramaphosa kwa kujitokeza mbele ya kamati hiyo na kukiri makosa ya ANC. "Ilikuwa muhimu kwa demokrasia kwa rais kukaa hapo na kujibu maswali kwa mchakato wa kimahakama kwa sababu hilo linatilia mkazo kuenea kwa utawala wa sheria na katiba juu ya mamlaka ya kisiasa," alisema mchambukizi wa kisiasa Onga Mtimka.

Mdadisi wa kisiasa Susan Booysen, alisema Ramaphosa aligeukia kukiri kushindwa kwa chama chake katika mambo mengi ili kuepuka kutoa ufafanuzi zaidi juu ya namna rushwa ilivyofanyika. "Tulimuona akikaribia kujitia hatiani mwenyewe, yumkini akimhusisha mwenzake yeyote katika ANC, au kuitia makosa ANC kwa namna hiyo," Booysen aliiambia DW.

Namna utekaji serikali ulivyotokea

Mwaka 2016, ripoti ya ofisi ya kupambana na rushwa ya Afrika Kusini iligundua kuwa afisa mtendaji mkuu wa zamani wa kampuni ya ugavi wa umeme Eskom, alikuwa amewasaidia kina Gupta kupata mkataba wa kununu kampuni ya Otimum Coal Holdings kutoka Glencore plc na aliwapa mikataba mizuri ya makaa ya mawe.

Ripoti hiyo ilifuatiwa na uvujishaji wa zaidi ya baruapepe 100,000 zilizofichua mawasiliano kati ya familia ya kina Gupta na kina Zuma kupitia kwa washirika, zikiainisha mtandao mgumu wa kandarasi za serikali, shuku za hongo, na utakatishaji fedha.

Barua pepe zilizovujishwa zilionesha kwamba mshirika wa kina Gupta alipata kiasia cha rand bilioni 5.3 (dola milioni 400) kutokana na kandarasi ya ugavi wa vichwa vya treni kwa kampuni ya taifa ya uendeshaji wa reli, Transnet SOC Ltd.

Kina Gupta wametuhumiwa pia kwa kushawishi uteuzi na utenguaji wa uteuzi wa mawaziri. Waziri wa fedha Nhlanhla Nene alipinga mipango ya Zuma kwa serikali kujenga viwanda ghali vya nyuklia na aliondolewa mwaka 2015.

Ndugu wawili,Ajay na Atul Gupta wakizungumza na vyombo vya habari mjini Johannesburg Machi 2011.Picha: Imago

Akina Guptas ni nani?

Atul, Ajay na Rajesh Gupta ni wafanyabiashara wa nchini Afrika Kusini waliokuwa na uhusiano wa karibu na Zuma na familia yake. Waliwasili kutoka India katika miaka ya 1990 na kuanzisha biashara ndogo ya computer kabla ya kununua hisa kubwa katika migodi ya urani, dhahabu na makaa ya mawe. Pia walianzisha nyumba ya kifahari ya wageni mbugani, kampuni ya uhandisi, gazeti na kituo cha televisheni kinachotangaza masaa 24.

Ndugu hao watatu waliripotiwa kuwa mabilionea katika sarafu ya taifa hilo ya rand. Atul Gupta aliorodheshwa na kampuni ya utafiti ya Who Owns Whom, kama mtu tajiri zaidi wa rangi nchini Afrika Kusini Desemba 2016, akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia rand bilioni 10.7.

Soma pia: Mashtaka dhidi ya Zuma kufufuliwa upya

Atul aliwasili Afrika Kusini akitokea jimbo la India la Uttar Pradesh mwaka 1993, akiuza viatu na computer kutokea buti la gari lake. Rajesh na Anjay walimfuata kaka yao, na mwaka 1997, familia hiyo, ambayo tayari ilikuwa na maslahi ya kibiashara nchini India, iliunda kampuni ya Sahara Computers.

Kina Gupta na kina Zuma

Mwaka 2007, Zuma alichaguliwa kuwa kiongozi wa ANC wakati sheria mpya zikifanya kuwa muhimu kwa kampuni kubwa kuwa na wakurugenzi weusi - hasa iwapo zilikuwa zinawania zabuni za serikali. Mtoto wa Zuma Duduzane alianza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 22 kama mkufunzi katika kampuni ya Sahara Computers, na alichaguliwa haraka kwenye bodi za kampuni kadhaa za kina Gupta.

Moja ya mabinti wa Zuma alikuwa mkurugenzi katika Sahara Computers, na mmoja wa wake zake alifanya kazi kwenye kampuni ya kina Gupta ya JIC Mining Services.

Zuma apandishwa kizimbani kwa ufisadi

01:05

This browser does not support the video element.

Soma pia: Cyril Ramaphosa ndiye rais mpya wa ANC

Duduzane pia aliripotiwa kuwa na hisa za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja katika mashirika kadhaa yanayomilikiwa na kina Gupta, ikiwemo Infinity Media, kampuni mama ya chaneli ya TV ya ANN7 na kampuni ya uchimbaji ya Tegeta Exploration & Resources.

Barua pepe za #GuptaLeaks hazijahakikiwa na vyanzo huru. Lakini bado, madai ya rushwa yamepelekea matumizi ya neno maarufu la "utekaji wa serikali" kuelezea ushawishi uliyovuka mipaka wa maslahi binafsi ya kibiashara ya kina Gupta kwenye taasisi za serikali.

Tume ya uchunguzi itaendelea kuwahoji watendaji wengine wa ANC. Ramaphosa anatarajiwa kurudi kwenye tume hiyo mwishoni mwa mwezi Mei kujibu mashtaka ya rushwa yaliotendwa na maafisa wa serikali wakati alipokuwa makamu wa rais chini ya Zuma.

Zuma mwenyewe amekataa kurejea kwenye tume hiyo na kujibu maswali zaidi, akisema bora aende gerezani kuliko kujipeleka kwenye mchakato uliosanifiswa kumtia kwenye uhalifu. Mpaka sasa, zaidi ya mashahidi 30 wamemhusisha na uovu kwenye tume hiyo.