Chama cha ANC chapania kubana uhuru wa vyombo vya habari
23 Septemba 2010Mkutano wa baraza kuu la chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini umeendelea leo ukituwama juu ya sera za sarafu ya randi na nia za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini humo. Chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress, ANC, kimepuuza miito ya makundi ya mrengo wa shoto yanayoitaka serikali ya rais Jacob Zuma kuipunguza thamani ya sarafu ya randi kwa kiwango kikubwa.
Chama hicho pia kimekataa kutilia maanani ushauri wa wanauchumi wanaotaka kuwepo mageuzi katika soko la ajira. Kamati ya chama cha ANC inayohusika na masuala ya uchumi ilitarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi kwenye kikao cha leo cha mkutano wa baraza kuu la kitaifa la chama hicho. Rais Zuma aliuambia mkutano huo siku ya Jumatatu kwamba anataka kuona sarafu ya Randi iliyo imara na inayoweza kuhimili mashindano katika soko la fedha la kimataifa.
Wajumbe wanasema kumekuwa na mjadala mkali kuhusu suala la kutaifisha migodi ya madini. Kitengo cha vijana wa ANC kimetaka migodi itaifishwe, lakini viongozi wa chama hicho wamesema uamuzi kuhusu sera hiyo utapiishwa mwaka 2012 wakati chama cha ANC kitakapofanya mkutano wake mkubwa.
Katika kikao cha jana chama cha ANC kilishinikiza kundwe jopo jipya litakaloadhibu tabia ya kuripoti habari zisizo sahihi, hatua ambayo imekosolewa vikali kama mpango unaolenga kuvikaba koo vyombo vya habari. Jopo la habari la chama hicho lilikutana faraghani kukamilisha vipengee vya mpango huo ambao umeungwa mkono na viongozi wa chama cha ANC.
Shirika la kimataifa la waandishi wa habari, CPJ, limesema sheria hizo zinafanana na zile zilizokuwepo wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi na huenda zikadumaza demokrasia nchini Afrika Kusini. Mashirika ya habari yanasema jopo hilo ni jaribio la kuwakandamiza waandishi wanaoandika habari za uchunguzi, ambao mara kwa mara hufichua visa vya rushwa na kuibebesha dhamana serikali, katika nchi ambako chama tawala cha ANC kina wingi wa karibu thuluthi mbili bungeni.
Lakini chama cha ANC kilichoongoza ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi, kimekanusha ukosoaji huo. Febe Potgieter-Gqubule, mwanachama wa ngazi ya juu wa chama hicho amesema, "Watu wengi walipoteza maisha yao wakati chama cha ANC kilipopigania uhuru wa vyombo vya habari. Hatutaufuja uhuru huo, lakini hakuna upeo mkubwa linapokuja suala la umilikaji wa vyombo vya habari na maoni yao."
Kwa upande mwingine bunge linatafakari muswada wa sheria ya vyombo vya habari ambao wabunge wa chama cha ANC wanasema unalenga kuzilinda siri za serikali. Vyombo vya habari vinaamini muswada huo unalenga kuzuia uchunguzi. Utakapopitishwa kuwa sheria, muswada huo utawazuia waandishi kupata taarifa kutoka kwa maafisa wa serikali na mashirika yanayomilikiwa na serikali. Wakosoaji wanasema muswada huo huenda ukawazuia wawekezaji kupata taarifa zinazoathiri hazina na masoko ya mabadilishano ya fedha za kigeni.
Mkutano wa chama cha ANC umepangwa kumalizika hapo kesho.
Mwandishi: Josephat Charo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman