1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ANC kuanza kuunda serikali ya mseto

2 Juni 2024

Chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress, ANC, Jumapili (02.06.2024) kimesema kitaanza mazungumzo na vyama vingine kuunda serikali mpya baada ya kupoteza wingi iliokuwa nao kwa miongo mitatu.

Cyril Ramaphosa, rais wa Afrika Kusini
Cyril Ramaphosa, rais wa Afrika KusiniPicha: Zhang Yudong/Xinhua/picture alliance

Huku asilimia 99.91 ya kura zikiwa zimehesabiwa kufuatia uchaguzi wa Jumatano, chama cha rais Cyril Ramaphosa cha ANC kilikuwa kimepata asilimia 40.2, matokeo ambayo ni mabaya kulinganisha na mwaka 2019 ambapo kilishinda asilimia 57.5 ya kura.

"Chama cha ANC kimejitolea kuunda serikali itakayodhihirisha ari ya umma, iliyo imara na inayoweza kuongoza barabara," alisema katibu mkuu wa chama hicho, Fikile Mbalula, wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari.

Chama cha ANC kinalazimika kuunda serikali ya mseto au angalau kiwashawishi wengine waunge mkono kuchaguliwa tena kwa rais Ramaphosa bungeni ili kumruhusu aunde serikali ya wachache.

Mbalula alisema chama cha ANC kitafanya mazungumzo ya ndani na pia makundi mengine katika siku chache zijazo.

Matokeo haya yanaashiria mageuzi makubwa kwa Afrika Kusini kwa kuwa chama hicho kimefurahia wingi bungeni tangu 1994, wakati shujaa wa ukombozi Nelson Mandela alipoiongoza nchi hiyo kutoka kwa utawala wa wazungu wachache na kuielekeza katika demokrasia.

"Matokeo haya yanatuma ujumbe wa wazi kwa chama cha ANC," alisema Mbalula. "Tungependa kuwahakikishia watu wa Afrika Kusini kwamba tumewasikia. Tumesikia wasiwasi wao, kufadhaika kwao na kutoridhika kwao," aliongeza.

Matokeo ya mwisho rasmi yanatangazwa Jumapili, huku rais Ramaphosa akitarajiwa kutoa hotuba kwa taifa wakati wa sherehe rasmi karibu na mji wa Johannesburg.

Madai ya mapungufu katika kujumuisha kura

Lakini baadhi ya vyama vya siasa vimedai kuna mapungufu katika uhesabuji na ujumuishaji wa kura. Chama kikubwa na chenye ushawishi cha rais wa zamani Jacob Zuma, uMkhono weSizwe (MK) kiliwaonya maafisa wa tume ya uchaguzi dhidi ya kusonga mbele na mchakato wa kuyatangaza matokeo ya mwisho.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: Thuso Khumalo/DW

"Kama hilo litatokea, mtakuwa mnatuchokoza," Zuma, mwenye umri wa miaka 82, alisema siku ya Jumamosi, akilalamika kuhusu masuala nyeti ambayo hakuyaeleza wala kuwasilisha ushahidi wa kuunga mkono madai yake.

Soma pia: ANC yaelekea kupoteza wingi wa kura Afrika Kusini

Data kutoka kwa tume huru ya uchaguzi ya Afrika Kusini, IEC, zimeonyesha chama cha MK kiko katika nafasi ya tatu na asilimia 14.59 ya kura, matokoe ya kushangaza kwa chama kilichoundwa miezi michache tu iliyopita kama chombo cha kumuwezesha rais wa zamani wa ANC Jacob Zuma kugombea katika uchaguzi.

Lakini wakati wote wa kampeni chama cha MK kiliwaambia wafuasi wake kingeshinda theluthi mbili ya kura. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Mosotho Moepya alisema tume hiyo itafuatilia na kuchunguza kila madai yaliyowasilishwa mbele yao na ilikuwa imeamuru kura zihesabiwe upya katika matukio 24.

Chama cha ANC sasa kitalazimika kugeukia wapinzani kutoka upande wa kushoto au kulia kuunda serikali. Chama kinachofuata siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Democratic Alliance, DA, kilishika nafasi ya pili na asilimia 21.78 ya kura, juu kidogo kulinganisha na matokeo kiliyoyapata katika uchaguzi wa 2019 ya asilimia 20.77.

Cha cha Democratic Alliance kinatawala jimbo la Western Cape na kimeahidi kufuatilia ajenda ya soko huru kinyume na tamaduni za chama cha ANC.

(afp)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW