1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMalawi

Chama cha Chilima chadai uchunguzi wa kuanguka ndege Malawi

13 Juni 2024

Chama cha makamu wa rais wa Malawi Saulos Chilima, aliyekufa wiki hii katika tukio la kuanguka ndege, leo kimedai uchunguzi ufanyike.

Makamu wa rais wa Malawi Saulos Chilima aliyefariki katika ajali ya ndege
Makamu wa rais wa Malawi Saulos Chilima aliyefariki katika ajali ya ndegePicha: Eldson Chagara/REUTERS TV

Chama cha United Transformation Movement - UTM, kiliungana na chama cha Rais Lazarus Chakwera cha Malawi Congress - MCP katika uchaguzi wa rais wa 2020, kwa kugombea kwa tiketi ya pamoja.

Lakini muungano huo uliviingiza vyama hivyo viwili madarakani upo chini ya shinikizo, huku viongozi wa UTM wakidai majibu kutoka kwa mawaziri wa serikali kuhusu ajali hiyo.

Kiongozi mwandamizi wa UTM gavana Stevie Mikaya, amesema wanataka kujua kilichofanyika kwa kiongozi wao.

Amesema ndege hiyo awali ilikuwa imesafiri kwenda Mzuzu chini ya mazingira sawa na hayo ya hali ya hewa. Alhamisi, wabunge wa UTM na madiwani wa chama walijaribu kumzuia Waziri wa Ulinzi Harry Mkandawire na Waziri wa Usalama wa Ndani Ken Zikhale Ng'oma kuhudhuria mazishi ya Chilima.

Kwenye makao makuu ya chama katika mji mkuu Lilongwe, Mikaya aliwatuhumu mawaziri hao kwa uzembe.