1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CDU cha Merkel chapata pigo chaguzi za majimbo

Josephat Charo
15 Machi 2021

Chama cha Christian Democratic Union cha kansela Angela Merkel wa Ujerumani kiko hali taabani Jumatatu (15.03.2021) baada ya kuangukia pua katika chaguzi za majimbo zilizofanyika jana Jumapili.

Deutschland Landtagswahl Baden-Württemberg
Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Wafuasi wa chama cha Kijani wanashangilia ushindi huku chama cha CDU kikiporomoka vibaya na kupata matokeo mabaya ya kihistoria chini ya mwenyekit wake mpya Armin Laschet, katika maeneo ambayo ni ngome zake za zamani, ikiwa ni miezi sita kabla uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi wa Septemba.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotolewa na maafisa baada ya kura zote kuhesabiwa chama cha CDU kilipata asilimia 24.1 ya kura katika jimbo la kusini magharibi la Baden-Wuerttemberg na kujikingia asilimia 27.7 ya kura katika jimbo jirani la Rhineland-Palatinate. Winfried Kretschmann wa chama cha Kijani ameshinda awamu ya tatu kama waziri mkuu wa jimbo la Baden-Wuerttemberg akipata asilimia 32.6 ya kura. Waziri mkuu maarufu wa chama cha Social Democratic SPD, Malu Dreyer ataendelea kuliongoza jimbo la Rhineland -Palatinate baada ya kushinda asilimia 35.7 ya kura.

Chama cha Kijani kimepata nguvu kutokana na matokeo hayo ya uchaguzi wa kwanza mwaka huu huku mahafidhina wakibaki wameduwaa. Katika majimbo yote mawili chama mbadala cha Ujerumani AfD kilifanya vibaya kuliko mwaka 2016, lakini kilifanikiwa kupata kati ya asilimia 10 na 11 ya kura. Chama cha FDP kimejikusanyia asilimia 11. 5 Baden-Würtemberg na asilimia 6.5 jimboni Rheinland-Palatinate.

Winfried Kretschmann, waziri mkuu wa jimbo la Baden-WuerttembergPicha: Marijan Murat/AFP

Kretschmann na Dreyer watabaki madarakani kwa miaka mingine mitano. Bi Dreyer alisema, "Kama nilivyowahi kusema awali, ushindi wa uchaguzi wa aina hii unampa kila mtu ari mpya. Bila shaka nimezungumza kwa akifupi na Olaf Scholz, mkuu wa chama cha Social Democratic SPD na nafurahi sana tunaweza kuonyesha furaha kwa wafuasi wote wa chama kila mahala na matokeo haya. Bil shaka ni muhimu sana tunapoelekea uchaguzi wa bunge.

Akizungumza baada ya kushinda uchaguzi waziri mkuu wa jimbo la Baden-Württemberg Winfried Kretschmann amesema sio tu janga la corona linalohitaji fikra mpya, weledi na bidii kutoka kwao. Pia amesema wana mwaka wa maamuzi mbele yao, majukumu makubwa yakiwa bayana - kulazimika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kusimamia vyema mageuzi ya kiuchumi na kulinda demokrasia ya kiliberali.

Kretschmann huenda akachagua kuendelea na serikali yake ya sasa ya mseto na chama cha CDU, au aunde mpya na chama cha SPD cha siasa za wastani zinazoegemea mrengo wa kushoto pamoja na chama kinachowapendela wafanyabiashara cha FDP ambavyo kila kimoja kilipata asilimia takriban 10 ya kura.

Chama cha CDU chaghadhabishwa na matokeo

Katibu mkuu wa chama cha CDU, Paul Ziemiak, amesikitishwa na matokeo akisema wangependelea kufanya vyema zaidi katika chaguzi za majimbo ya Baden-Wuerttemberg na Rhineland-Palatinate, lakini chombo kilikwenda mrama.

"Tabia mbaya isiyokubalika na ya aibu ya wabunge binafsi imehakikisha kuwa katika duru ya mwisho ya kampeni ya uchaguzi, ilileta upepo wa aibu na changamoto usoni mwa waandaaji wa kampeni. Hali hiyo haikuwa nzuri na kusababisha shinikizo kubwa kwa kampeni ya uchaguzi."

Kauli yake imeungwa mkono na Norbert Roettgen wa chama cha CDU aliyesema matokeo hayo yanasikitisha kwa chama hicho katika maeneo ambayo ni ngome zao za zamani na wanahitaji kujiuliza sababu ya matokeo hayo ni zipi. Roettgen amesema wanahitaji kujitathmini na kujikosoa wenyewe.

Matokeo haya yanakuja huku kukiwa na hisia za kutoridhika na serikali za majimbo yote mawili kuhusu sheria na taratibu za kuzuia na kufungia shughuli za kila siku kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Akizungumza na kituo cha televisheni ya umma cha ARD jana Jumapili, Wolfgang Schäuble, spika wa bunge la Ujerumani na mwanachama wa chama cha CDU cha kansela Merkel amesema wapiga kura wamechagua watu badala ya vyama na janga la corona limewasaidia wagombea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW