1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Die Linke chashinda Thuringia

Yusra Buwayhid
28 Oktoba 2019

Chama cha siasa za mrengo wa kushoto Ujerumani, Die Linke, kimeshinda uchaguzi wa jimbo la Thuringia Jumapili. Chama cha kizalendo AfD, kimeshika nafasi ya pili na kukiwacha nyuma chama cha Kansela Angela Merkel, CDU.

Deutschland Landtagswahl in Thüringen - Linke
Picha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Kulingana na matokeo rasmi, chama cha Die Linke kimeshinda asilimia 31 ya kura zote zilizopigwa, na kukifanya kuwa chama cha kisiasa chenye nguvu jimboni humo kwa mara ya kwanza.

Bodo Ramelow, mgombea wa chama cha Die Linke na mkuu wa sasa wa serikali ya jimbo la Thuringia amesema ushindi wao ni ushahidi wa kukubalika na umma.

"Miaka mitano iliyopita, hawakufikiria tungeweza kufanya kazi, walidhani tutashindwa baada ya siku 100 na, miaka mitano baadaye, bado tuko hapa na tunasema tutaendelea!"

Uchaguzi huo wa jana Jumapili katika jimbo hilo ndogo la Ujerumani Mashariki ulikuwa mtihani mkubwa kwa chama cha AfD, ambacho wafuasi wake walikipigia kura kwa wingi.

Ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2014, chama cha AfD kimeongeza kura maradufu hadi asilimia 23.4, na kukipita chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU. Ushindi huo unakifanya chama cha AfD kuibuka kama chama cha pili chenye nguvu katika bunge la jimbo la Thuringia.

Bodo Ramelow, katika uchaguzi wa jimbo la Ujerumani huko ThuringiaPicha: picture-alliance/dpa/F. May

Mazungumzo magumu ya kuunda serikali

Chama cha kihafidhina cha CDU kimepoteza kura nyingi katika uchaguzi wa jana. Kimepata asilimia 21.8 ya kura zote zilizopigwa. Na kupoteza zaidi ya asilimia 11. Chama cha SPD kimepoteza kura nyingi zaidi. Kimepata asilimia 8.2 ya kura, ikilinganiswha na asilimia 12.4 ya mwaka 2014.

Chama cha Kijani kinachopigania mazingira, ambacho kinaunda serikali ya mseto jimboni humo pamoja na Die Linke na SPD, pia kimepoteza uungwaji mkono na kupata asilimia 5.2 ya kura na kupindukia kidogo asilimia 5 ya kuweza kuingia bungeni.

Waziri Mkuu wa Thuringia Bodo Ramelow kiongozi wa kwanza wa Die Linke kuiongoza serikali ya jimbo la Ujerumani mnamo mwaka 2014, atakabiliwa na mazungumzo magumu mbele yake ya kuunda serikali ya mseto.

Matokeo rasmi yanathibitisha kwamba muungano wa awali wa Die Linke, chama cha Kijani na SPD hautapata wingi wa viti katika bunge la mjini Erfurt.

Gazeti la Ujerumani la Heilbronner Stimme linaelezea matokeo ya uchaguzi huko Thuringia kama janga kwa vyama vikuu vya kisiasa. Gazeti hilo kutoka mji wa Heilbronn wa jimbo la Baden-Wuerttemberg limeandika kwamba vyama CDU na SPD vimepata matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi katika jimbo la Thuringia.

dpa,afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW