1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Ennahda chataka mdahalo nchini Tunisia

Sylvia Mwehozi
27 Julai 2021

Chama kikubwa nchini Tunisia cha Ennahda kimeitisha mazungumzo ya kisiasa yatakayoitoa nchi hiyo katika mgogoro baada ya kumshutumu rais Kais Saeid kwa mapinduzi wakati alipomfuta kazi waziri mkuu na kulivunja bunge. 

Tunesien Tunis | Demonstration der islamischen Ennahda-Partei
Picha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Taarifa hiyo imetolewa wakati chama hicho cha Kiislamu chenye mrengo wa wastani kikitoa maelekezo kwa wafuasi wake kupitia matawi ya chama kutopiga kambi tena nje ya bunge na kuepuka maandamano. Taarifa hiyo inakinzana na ile iliyotolewa awali na kiongozi wake Rached Ghannouchi ambaye aliwahimiza wafuasi wake kuingia barabarani.

Ingawa baadhi ya viongozi waandamizi walitaka kuendeleza maandamano, lakini viongozi wake wameamua kuepuka mivutano zaidi na kuruhusu kipindi cha utulivu, kulingana na maafisa wawili ndani ya chama. Eneo la nje la bunge, ambako siku ya Jumatatu kulikuwa na makabiliano baina ya wafuasi wa Ennahda na wale wa rais Kais Saeid, siku ya Jumanne lilikuwa tupu.

Tunisia inakabiliwa na mgogoro mkubwa tangu mapinduzi ya mwaka 2011 ambayo yalianzisha demokrasia. Rais Saeid alisema kuwa uamuzi wake ulikuwa halali kulingana na katiba inayoruhusu hatua zisizokuwa za kawaida wakati wa dharura.

Rais wa Tunisia Kais Saied na maafisa waandamizi wa kijeshiPicha: Tunisian Presidency/Handout/AA/picture alliance

Chama cha Ennahda na vyama vingine vitatu vikubwa bungeni vyote vimelaani hatua hiyo ni kuiita kuwa ni mapinduzi. Zipo taarifa kuwa nchi jirani ya Algeria imewahimiza Saied na wapinzani wake kuepusha mivutano au wategemee uingiliaji kati wa nguvu kutoka nje. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alizungumza na rais Saied Jumatatu jioni na kumtaka "kuheshimu misingi ya demokrasia na haki za binadamu". Nabila Massrali ni msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya na amesema kuwa; "Umoja wa Ulaya unafuatilia kwa karibu hali inayoendelea Tunisia. Ni wazi kwamba katika taarifa yetu, Umoja wa Ulaya unaunga mkono utawala wa sheria, demokrasia na misingi ya haki za binadamu. Tunatoa wito wa nchi kurejea katika hali ya kawaida wa shughuli za kitaasisi."

Saied bado hajatangaza waziri mkuu mpya wa mpito na amesema kuwa atambadilisha waziri wa ulinzi, ingawa hajasema ikiwa kutakuwa na mabadiliko kamili ya baraza la mawaziri.

Wakati huohuo kundi la mashirika makuu ya kiraia ikiwemo chama cha wafanyakazi kilicho na nguvu, yamemuonya rais Saied kutopanua hatua alizotangaza siku ya Jumapili kupindukia mwezi mmoja. Kwenye taarifa yake, kundi hilo linalojumisha pia waandishi wa habari, mawakili na yale ya haki za binadamu, limemtaka rais Saied kutoa mwongozo shirikishi kwa ajili ya kutatua mgogoro.