Chama cha Kansela wa Ujerumani chashindwa uchaguzi wa Berlin
13 Februari 2023Kwa mara ya kwanza katika miongo miwili, chama hicho kimeshika nambari ya pili baada ya chama cha upinzani CDU katika jimbo hilo. Chama cha Scholz kimekuwa kikishikilia kiti cha meya wa mji wa Berlin tangu mwaka 2001.
Hata hivyo bado haiko wazi iwapo mgombea wa CDU Kai Wegner ataongoza jimbo hilo la mji mkuu. Kutegemea matokeo ya mwisho, chama cha Kijani na SPD, vinaweza kuendeleza muungano wao wa sasa kwa kuungana na chama cha tatu.
Japo uchaguzi huo uliegemea zaidi masuala yanayowaathiri wakaazi wa jimbo hilo, kushindwa kwa chama cha Scholz kunajiri mnamo wakati kuna ukosoaji mkubwa dhidi yake, kuhusu kukawia kwake kutoa misaada ya kijeshi kwa Ukraine iliyovamiwa na Urusi mwaka uliopita. Mahakama ya kikatiba iliamuru uchaguzi wa jimbo hilo kurudiwa kwa kuwa haukushughulikiwa vyema mwaka 2021.