Chama cha kiliberali FDP chajipatia uongozi mpya
11 Mei 2011Waziri wa uchumi Rainer Brüderle ameteuliwa kuongoza kundi la chama cha FDP katika bunge la shirikisho-Bundestag. Waliberali wanajaribu kujipendekeza tena kwa wapiga kura baada ya kuporomoka chini ya kiwango cha asili mia tano ya kura kufuatia uchambuzi wa maoni ya umma wa hivi karibuni-pigo kubwa ikilinganishwa na asili mia 14 ya kura walizojipatia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.
Uamuzi wa kumpokonya uongozi wa kundi la FDP bungeni mwanasiasa aliyepoteza imani ya wapiga kura wa chama hicho cha kiliberali, Bibi Birgit Homburger, umefuatia miezi kadhaa ya mivutano kati yake na wakuu wenzake chamani.
Mvutano ndani ya chama hicho cha kiliberali ndio chanzo cha kuachana waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu, Guido Westerwelle, na wadhifa wake kama mwenyekiti wa FDP mwezi uliopita.
Mabadaliko hayo yamejiri siku chache kabla ya FDP kuitisha mkutano wake mkuu ijumaa ijayo mjini Rostock.
"Hali ni ngumu" amekiri mwenyekiti mpya wa chama cha FDP, Philipp Rösler, mwenye umri wa miaka 38, wakati wa mazungumzo pamoja na waandishi habari mjini Berlin. Ameongeza kusema hata hivyo:
"Ninajua kwa jinsi gani, kwa ushirikiano pamoja na wenzangu chamani, tutakavyoweza kukitoa chama cha FDP katika hali hii ngumu. Na ndio maana ninamshukuru kwa dhati Birgit Homburger, kwa sababu uamuzi wake wa kuachana na wadhifa wake ndio utakaonisaidia kutekeleza fikra niliyo nayo kwa masilahi jumla ya chama cha FDP."
Philipp Rösler, ambae kwa sasa ndie waziri wa afya wa serikali kuu, atakabidhiwa wadhifa wa waziri wa uchumi -na wizara ya afya inatazamiwa kuongozwa na mwanasiasa kijana zaidi, Daniel Bahr, mwenye umri wa miaka 34, mwenyekiti wa FDP katika jimbo la North Rhine Westphalia.
Waliberali wamekumbwa na mkosi mwengine jana baada ya gazeti la mjini Berlin kufichua kwamba chuo kikuu mashuhuri cha Heidelberg kinapanga kumpokonya hadhi udaktari kwa tuhuma za udanganyifu, Silvana Koch-Mehrin, mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika chama hicho cha kiliberali.
Mwandisghi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/afp,dpa
Mhariri: Miraji Othman