1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Merkel chapigwa kumbo uchaguzi wa jimbo

Sylvia Mwehozi5 Septemba 2016

Chama cha Kansela Angela Merkel wa Ujerumani cha Christian Democratic CDU kimepoteza nafasi yake kama chama cha pili chenye nguvu katika uchaguzi wa Mecklenburg-Vorpommern uliofanyika siku ya Jumapili.

China G20 Gipfel in Hangzhou - Angela Merkel
Picha: Getty Images/AFP/J. Eisele

Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya uchaguzi yaliyotolewa chama kinachopinga wahamiaji cha mbadala kwa Ujerumani AfD, kimeibuka nafasi ya pili.

AfD imepata kura asilimia 20.8, ikimaniisha kwamba chama hicho kitaingia bunge la jimbo hilo la kaskazini mashariki kwa mara ya kwanza. Tayari kimeshapata wawakilishi katika majimbo mengine nane na hii ikiashiria kwamba kinaweza kuingia katika bunge la taifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani. CDU imeibuka na asilimia 19 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo uliotabiriwa kwa kiwango kikubwa kuwa ungekuwa ni mtihani mpya kwa sera za Bi. Merkel zenye utata kuhusu mgogoro wa wakimbizi.

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD ambacho kwa hivi sasa kinaongoza Muungano mkuu na CDU kama mshirika wake mdogo, kimesalia kuwa chama chenye nguvu baada ya kupata asilimia 30.6. Matokeo yanamaanisha kwamba, licha ya vyama vyote ambayvo vinaongoza serikali kupoteza, SPD na CDU bado vitaweza kuunda Muungano kwa kipindi cha miaka mitano. Ingawa mshindi wa uchaguzi huo kutoka chama cha SPD Erwin Sellering hajasema ikiwa atataka kuungana tena na CDU.

Mshindi wa uchaguzi wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern Erwin Sellering wa SPDPicha: picture-alliance/dpa/B. Wüstneck

Sera ya wakimbizi yachangia

Kiongozi wa chama cha AfD Frauke Petry amesema mafanikio waliyoyapata katika uchaguzi huo wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern ambalo ni nyumbani kwa jimbo la uchaguzi la Kansela Merkel la Stralsund, ni matokeo ya "janga la sera ya wakimbizi" akiongeza kwamba "tumeiweka CDU sehemu inakostahili".

Katibu mkuu wa CDU Peter Tauber amesema kuanguka kwa chama chao kumetokea kwa sababu kumekuwa na ongezeko la "kutoridhishwa na upinzani" dhidi ya uamuzi wa Merkel wa kutoifunga mipaka ya Ujerumani dhidi ya wakimbizi.

Matokeo hayo pia yameashiria ukweli kwamba AfD imegawana kura miongoni mwa vyama na kwamba asilimia 34 ya wafuasi wake hawakupiga kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2011. Uungwaji mkono wa umma kwa bi Merkel ulishuka wakati wa mashambulizi mawili ya kigaidi ya mwezi Julai yaliyotekelezwa na waomba hifadhi na kudaiwa kufanywa na kundi linalojiita dola la Kiislamu IS. Wakosoaji wa uamuzi wake wa kutofunga mipaka ya Ujerumani ambao ulishuhudia kuwasili kwa wakimbizi milioni 1.1 kwa mwaka 2015, wanasema Merkel ni wa kulaumiwa kwa kuleta kitisho cha usalama nchini Ujerumani.

Wafuasi wa AfD wakishangilia matokeo ya uchaguziPicha: Reuters/H. Hanschke

Mwanachama mmoja wa CDU Klaus Dieter Arlt amesema matokeo haya waliyatarjia. "Matokeo haya hayashangazi bali yanakatisha tamaa. Yamedhihirisha kuwa vyama vikuu viwili, CDU na SPD havijaweza kutatua matatizo ya watu".

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kabla ya uchaguzi na Infratest Dimap, zaidi ya theluthi tatu ya wapiga kura wa Mecklenburg-Vorpommern walisema kwamba utitiri wa wakimbzii ungekuwa ni kigezo cha maamuzi siku ya upigaji kura.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW