1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Putin chaelekea ushindi uchaguzi wa bunge

19 Septemba 2021

Warusi wamepiga kura kwenye siku ya mwisho ya uchaguzi wa ubunge uliofanyika kwa siku tatu katika taifa hilo lenye maeneo 11 yenye majira tafauti ya nyakati, huku chama cha Rais Vladimir Putin kikitazamiwa kushinda.

Russland Moskau | Parlamentswahl
Picha: Artyom Geodakyan/TASS/picture alliance

Chama kinachomuunga mkono Rais Vladimir Putin, United Russia, kinatazamiwa kupata ushindi mkubwa, baada ya serikali kufanikiwa kuliangamiza vuguvugu la kiongozi mkuu wa upinzani, Alexei Navalny na kuwazuwia wapinzani kuwania. 

Ushindi huo unaotarajiwa utatumiwa na Ikulu ya Kremlin kama ithibati ya jinsi Rais Putin anavyoungwa mkono licha ya hali ngumu ya uchumi kuendelea kuwaathiri raia wa nchi hiyo.

Chama cha United Russia kinamuunga mkono Putin, mwenye umri wa miaka 68, ambaye licha ya umashuhuri wake kushuka, bado ndiye anayefahamika zaidi miongoni mwa wapinzani wake kwenye karatasi ya kura - Chama cha Kikomunisti na kile cha cha kihafidhina, LDDR, ambacho mara nyingi huunga mkono serikali.

Kwa sasa, United Russia ina takribani robo tatu ya bunge kuu la taifa, Duma, lenye vita 450. Hiyo iliisaidia Kremlin kupitisha mabadiliko ya kikatiba ambayo yanamruhusu Putin kuwania kwa miongo mingine miwili zaidi baada ya mwaka 2021, ikimaanisha kuwa anaweza kusalia madarakani hadi mwaka 2036.

"Ikiwa United Russia itashinda, nchi yetu inaweza kutarajia miaka mingine mitano ya umasikini, miaka mitano ya ukandamizaji, miaka mitano iliyopotea," unasema ujumbe wa Navalny kwa wafuasi wake.

Washirika wa Navalny wazuiwa

Mmoja wa wapigakura wakiweka kura zao katika uchaguzi wa bunge wa Urusi.Picha: Erik Romanenko/TASS/dpa/picture alliance

Washirika wa Navalny walizuiwa kuwania baada ya vuguvugu lake kupigwa marufuku mwezi Juni kwa madai ya kuwa kundi la siasa kali. Viongozi wengine wa upinzani wanadai kuandamwa kwa mbinu za kampeni chafu.    

Mfanyabiashara mkubwa kutoka chama cha Kikomunsti anasema alizuiwa kuwania kinyume na sheria, huku mgombea mmoja wa kiliberali katika mji wa St. Petersburg akisema majina mawili yanayofanana na yake yaliwekwa ili kuwababaisha wapigakura.  

Lakini ikulu ya Kremlin inakanusha ukandamizaji unaofanywa kwa nia za kisiasa na badala yake inasema watu wanahukumiwa kwa mujibu wa sheria walizozivunja. Ikulu hiyo na chama cha United Russia wanakanusha kuhusika na mchakato wa kuwasajili wagombea.

Kambi ya Navalny ilitumia mbinu ya kumshinda Rais Putin kwa kuwataka wapiga kura kuwachaguwa wagombea walioonesha upinzani mkali kwa wale wa United Russia, lakini mamlaka nchini Urusi zimekuwa zikijaribu kuzuwia kampeni hiyo kufanikiwa.

"Siku moja, tutaishi kwenye Urusi ambapo itawezekana kuwapigia kura wagombea wazuri walio kwenye majukwaa tafauti ya kisiasa," alisema mshirika wa Navalny, Leonid Volkov, kupitia mtandao wa Telegram.   
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW