Chama cha RCD kusimamisha operesheni Tunisia
7 Februari 2011Hatua hiyo imechukuliwa baada ya maandamano mapya kuzuka ya kuwapinga baadhi ya viongozi wa zamani wanaoshiriki kwenye serikali mpya ya muda iliyoteuliwa.Tunisia iligubikwa na maandamano ya ghasia mwezi uliopita yaliyomsababisha Rais wa zamani Ben Ali kukimbia na serikali kusambaratika.
Mabadiliko hayo yalitangazwa na Waziri wa mambo ya ndani wa Tunisia,Fahrat Rajhi,aliyeitoa taarifa hiyo kwenye kituo cha televisheni ya taifa.Chama cha Kidemokrasia cha Tunisia,RCD,cha rais aliyeng'olewa madarkani Zine El Abidine Ben Ali kimeamriwa kuzisimamisha operesheni zake kwa muda na kuzifunga afisi zake kote nchini humo.
Ahadi na vitendo
Kulingana na taarifa hiyo ya Waziri wa mambo ya ndani,azma ya hatua hiyo ni kuvizuwia vitendo vyovyote vinavyokiuka sheria na kuivuruga hali nzima ya taifa.Kutokana na hilo,chama cha RCD kimeamriwa kutoandaa mikutano ya aina yoyote ile.
Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya ndani,hatua hizo zimechukuliwa wakati ambapo ombi rasmi limeshawasilishwa mahakamani ili kuitaka ikisambaratishe chama hicho tawala cha zamani.Ili kuipa uzito hatua hiyo,Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton,"alimsisitizia waziri kuwa tunawaunga mkono ili waweze kuwa na kipindi cha mpito kinachojikita katika demokrasia kadhalika tunataraji serikali hii itazitimiza ahadi zake kwa vitendo."
Kopo la gesi
Duru nyengine zinaeleza kuwa mvulana mmoja aliuawa jana usiku katika mji wa Kebili ulio kusini mwa Tunisia pale aliporushiwa kopo la gesi ya machozi wakati wa mapambano ya ghasia kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.Kulingana na shirika la habari la taifa,TAP,maafisa hao walilazimika kuingilia kati baada ya genge la vijana kukivamia kituo cha polisi wa taifa na kujaribu kukitia moto.
Taarifa hizo zinaeleza pia kuwa baadhi ya waandamanaji walikusanyika siku ya Jumamosi nje ya afisi ya gavana mjini Kebili ili kuupinga uteuzi wa gavana mpya.Hali hiyo iliwalazimu wanajeshi kupiga doria mjini Kef ulio eneo la magharibi ambako watu wanne wanaripotiwa kuwa waliuawa siku moja kabla, baada ya kituo kiomja cha polisi kuteketezwa wakati wa maandamano mapya.Hata hivyo hali ni shwari na genge hilo la wahalifu limetoweka mtaani ,kama anavyoeleza mwanaharakati wa kutetea masuala ya ajira,Raouf Hadaoui.
Kutelekeza majukumu
Kulingana na duru za wizara ya mambo ya ndani,watu wawili waliuawa na wengine 13 walijeruhiwa katika ghasia hizo za wikendi zilizotokea mjini Kef.Kwa upande wake,shirika la habari la TAP limeeleza kuwa waandamanaji hao wanamtaka mkuu wa polisi wa eneo la Kef ajiuzulu kwasababu ya matumizi mabaya ya madaraka.
Wakati huohuo,kiongozi wa ujumbe wa Bunge la Umoja wa Ulaya unaouzuru mji wa Tunis,Jose Ignacio Salafranca,ametoa wito wa uchunguzi kufanywa ili kuwatambua wahalifu hao wa Kef.
Gavana mpya wa mji wa Gafsa naye pia alilazimika kuyatelekeza majukumu yake baada ya kuvamiwa na waandamanaji waliomshinikiza ajiuzulu.
Kwa upande wake,serikali ya mpito ya Tunisia iliwateua magavana hao na wakuu wa polisi wapya katika mikoa yote 24 kama njia moja ya kuituliza hali nchini humo.Uteuzi huo ulifanyika siku chache zilizopita.
Hata hivyo,waandamanaji na wanasiasa wa upinzani wanataka mabadiliko mengi zaidi uongozini kwani wanadai kuwa baadhi ya walioteuliwa upya wana mafungamano na serikali iliyong'olewa madarakani.Moncef Marzouki ni mwanasiasa wa upinzani na anashikilia kuwa hakuna mabadiliko kwani
,"Tumemuondoa dikteta mwenyewe ila udikteta bado upo.Maafisa wa ujasusi bado wapo,chama kilichojikita kwenye udikteta bado kipo."
Sidi Bouzid
Shirika la habari la TAP limefafanua kuwa maafisa wawili wa kijeshi wamekamatwa kwasababu ya tuhuma za mauaji ya watu wawili waliokuwa wanazuiliwa eneo la Sidi Bouzid lililo katikati mwa Tunisia.Maandamano hayo ya ghasia yalianzia mtaa wa Sidi Bouzid pale Mohammed Boauzizi kuuawa baada ya kujiteketeza kwa moto tarehe 17 mwezi wa Disemba.
Tunisia bado inaendelea kutatizika kisiasa hata baada ya Rais wa zamani Ben Ali kung'olewa madarakani kiasi ya wiki tatu zilizopita.Ghasia hizo za kumshinikiza aondoke madarakani zimesababisha wimbi la maandamano ya kudai mageuzi katika eneo la Maghreb ili kuulazimisha uongozi wa kidikteta usiodumisha demokrasia kuondoka.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE
Mhariri: Mtullya Abdu