Chama cha siasa kilichojitenga na chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini chashinda chaguzi ndogo.
11 Desemba 2008Uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Magharibi la Cape ulionekana kama kipimo cha kukiunga mkono chama hicho cha Congress of the People(COPE), kilichoundwa baada ya viongozi wa juu kujiondoa katika chama tawala cha African National Congress(ANC), kwa kitendo chao cha kupinga kulazimishwa kujiuzulu kwa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.
Wagombea wa chama hicho cha COPE walisimama kama wagombea binafsi katika uchaguzi huo uliofanyika Jumatano kwa sababu chama hicho bado hakijasajiliwa rasmi kama chama cha siasa. Chama hicho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 6, mwezi huu.
Moeletsi Mbeki, mchunguzi wa masuala ya kisiasa na kaka wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema ushindi wa chama hicho ambacho bado hakijazinduliwa rasmi unaonyesha mwelekeo mzuri.
Afisa wa uchaguzi wa eneo hilo, Courtney Sampson, amesema katika uchaguzi huo chama tawala cha ANC kimeshinda viti vitatu, chama cha COPE kimeshinda viti 10, chama cha upinzani cha Democratic Alliance kimeshinda viti 9 na wagombea binafsi wa chama cha Democrats wameshinda viti vitano vya majimbo 27 yaliyokuwa yakishindaniwa.
ANC hakikugombania majimbo 12 ya jimbo la Magharibi la Cape, kituo kikubwa cha utalii nchini Afrika Kusini, baada ya kuzuiwa na tume ya uchaguzi kwa kushindwa kuwaandikisha wagombea wao katika muda muafaka.
Moeletsi Mbeki amesema chama cha COPE kilihitaji kushinda asilimia tano ya kura katika kiwango cha taifa ili kuaminika kisiasa. Kwa upande wake Helen Zille, kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance, amesema matokeo ya uchaguzi huo mdogo yameonyesha kuwa chama cha COPE kinasambaratisha kura za ANC.
Msemaji wa ANC, Garth Strachan amesema matokeo hayo yanakatisha tamaa, akiongeza kuwa chama hicho kinahitaji kuongeza nguvu zaidi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. ANC kimekuwa chama tawala nchini Afrika Kusini tangu mwaka 1994 ulipomalizika utawala wa kibaguzi, lakini nguvu za kutawala za chama hicho zinakabiliwa na changamoto ya mgawanyiko pamoja na kesi ya rushwa inayomkabili kiongozi wake, Jacob Zuma.
Bwana Zuma amesema chama cha COPE hakiaminiki kwa wananchi, lakini maafisa wa ANC wana wasi wasi kuhusu kujiondoa kwa wajumbe wengine na wameenda mahakamani kuzuia chama hicho kilichojitenga kutumia jina la Congress of the People.
Chama cha COPE kina mpango wa kugombea viti vya bunge katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka ujao wa 2009. Tangu mwaka 1994, ANC hakijafanikiwa kushinda viti vingi katika jimbo la Magharibi la Cape ambako chama cha upinzani cha Democratic Alliance kinatawala katika mji wa Cape Town.