1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Upinzani Myanmar chavunjwa

7 Mei 2010

Chama cha upinzani cha mwanasiasa maarufu Aung San Suu Kyi nchini Myanmar kimevunjwa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu baadae mwaka huu lakini wanachama wa chama hicho wamesema wataunda chama kipya.

Kiongozi wa chama cha upinzani Myanmar NLD Aung San Suu KyiPicha: AP

Chama cha The National League for democracy kilivunjwa usiku wa kuamkia leo baada ya kushindwa kujiandikisha kama chama cha kisiasa hadi kufikia tarehe 6. Kwa usemi mwingine chama hicho kilikataa kujiandikisha hadi hiyo jana.

Msemaji wake Nyan Win ameeleza kwamba kujiandikisha kwa chama chake kungelikuwa na maana ya kumfukuza kiongozi wao San Suu Kyi na kuususia uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mnamo mwaka huu.

Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza kufanyika nchini Myanmar baada ya miaka 20. Msemaji huyo pia ameeleza kwamba uamuzi wa kutojiandikisha umesababishwa na sheria ya dhulma ya utawala wa kijeshi.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama cha National League for democracy,NLD Win Hlaing amesema kutokana na sheria hiyo, hakuna mtu anaeweza kutarajia kuyaona matokeo ya haki ya uchaguzi huo.Amesema kutokana na sheria hiyo hapatakuwa na uwezekano wa kujenga demokrasia ya kweli nchini.


Bila ya upinzani wenye nguvu haitawezekana kujenga demokrasia ya dhati.Utawala wa kijeshi unajaribu kusababisha mazingira yatakayozuia kuwakilishwa kwa vyama vya upinzani bungeni."

Kiongozi wa chama cha the national league for democracy bibi Aung San Suu Kyia alikishauri chama chake kutoshiriki katika uchaguzi.

Katika muda wa miaka zaidi ya 14 kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha The National League for Democracy san suu kyi amekuwa anazuiliwa nyumbani kwake au jela.

Sheria mpya ya uchaguzi ya utawala wa kijeshi wa Myanmar imeshutumiwa vikali duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki moon ameutaka utawala wa kijeshi wa Myanmar uandae uchaguzi huru na wa haki na kumshirikisha kiongozi wa upinzani bibi Aung San Suu Kyi .

Katibu Mkuu Ban ameeleza kuwa katika mazingira ya sasa huenda matokeo ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika, yasitambuliwe.

Lakini maafisa wa utawala wa kijeshi wa Myanmar wameliambia shirika laa habari la AFP kuwa chama cha bibi San Suu Kyi hakina uhalali tena.

Hatahivyo wanachama wa NLD wamesema wataunda chama kipya cha upinzani.

Mwanaharakati maaruf wa haki za binadamu Win Tin aliekuwa mwanachama mwandamizi wa chama cha NLD amesema kuvunjwa kwa chama chama NLD siyo jamb la kusikitisha, na ameeleza kwamba chama chao kingelipoteza uadilifu wake laiti kingelikubali masharti y utawala wa kijeshi.Lakini mwanaharati huyo amesisitiza kwamba kuvunjwa kwa chama cha NLDsiyo mwisho wa harakati za kupigania demokrasia nchini Myanmar.

Chama cha The National League for democracy kiliundwa m namo mwaka 1988 kufuatia harakati upinzani mkubwa dhidi ya utawala wa Mynmar zilizosababisha kuuawa kwa maalfu ya wapinzani. Mnamo mwaka 1990 chama hicho kilishinda uchaguzi mkuu kwa kishindo, lakini matokeo ya uchaguzi huo hayakutambuliwa na utawala wa kijeshi.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/ZA

Mhariri/.Aboubakary Liongo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW