Chama cha Victor Orban chasimamishwa katika bunge la Ulaya
21 Machi 2019Miongoni mwa yaliyoandikwa na wahariri ni pamoja na kusimamishwa katika kundi lenye nguvu EPP katika bunge la ulaya kwa chama cha Fidesz cha Hungary kinachoongozwa na waziri mkuu Victor Orban,Na kurefushwa marufuku ya Ujerumani kuiuzia silaha Saudi Arabia.
«Augsburger Allgemeine».Limeandika kuhusu kutimuliwa kwa chama cha waziri mkuu Victor Orban katika bunge la Umoja wa Ulaya.
Katikati ya kampeini ya uchaguzi wa bunge la Ulaya,chama cha wahafidhina cha Christian Democrats kimeingia katika mapambano dhidi ya upande wa siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia na upande wa siasa za mrengo wa shoto ukitaka kuongoza na Viktor Orban kubakia kuwa kama farasi aliyeshindwa katika mbio za mapambano yake.Lakini waziri mkuu huyo wa Hungary mpaka dakika ya mwisho ameendelea kubakia mkaidi na kujiona mjini Brussels kama ni mshindi.Kwamba pia anataka kulifukuza jopo la watu watatu la kundi la chama chake mwenyewe ni jambo lililomfanya kufedheheka hasa. Orban kupinga kufukuzwa chama chake katika muungano wa EPP sio habari njema. Hisia zake zimeonesha wazi kwamba hajifunzi na wala haondoki.
Gazeti la «Mannheimer Morgen» limeandika kuhusu mpango wa waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz wa kubana matumizi katika bajeti ya mwaka 2020.
Waziri wa fedha Scholz anataka fedha zinazotolewa kwa wakimbizi kwa kipindi cha miaka mitano ya mwanzo baada ya kukubaliwa nchini Ujerumani zitolewe kwa mara moja kwa mkupuo kwa kila mkimbizi. Mpango huu lakini ni mpya kabisa duniani. Watoto wa wakimbizi wanalazimika kila siku kwenda chekechea au shule. Na hata mchakato wa kuwajumuisha katika soko la ajira nchini Ujerumani unachukuwa muda mrefu. Wengi wa wanaoomba hifadhi wanabidi pia kujumuishwa katika shughuli za kazi za kijamii au kushiriki katika kupata ushauri nasaha kutokana na kiwewe cha vita na ugaidi.Bila shaka hilo haliwezi kuhesabiwa kama kitu kinachoteremsha kiwango cha kodi katika uchumi.
«Weser-Kurier» linalochapishwa mjini (Bremen) ,limeandika juu ya biashara ya kuiuzia silaha Saudi Arabia
Inavyoonesha haitoshi bado mfalme Salman wa Saudi Arabia aliyoyafanya kipindi cha miezi kadhaa na miaka iliyopita,mpaka kushindwa kutompa silaha za maangamizi ya watu zinazotengenezwa Ujerumani. Bin Salman ameshambulia kwa mabomu nchini Yemen na raia wengi kuuwawa.Anazikanyaga kwa miguu haki za binadamu,bila ya kusahau mauaji mabaya aliyoyafanya ya mwandishi habari Jamal Khashogi na sio hayo tu bali anaendesha utekaji nyara,kuisusia nchi jirani yake ya Qatar na kama inavyoonekana kuingia kwake kwenye siasa kunamfanya kujisogeza zaidi na zaidi katika vita na Iran.Wakati bunge la Ujerumani likifikiria kupiga marufuku kuiuzia silaha Saudi Arabia kulijitokeza ukosoaji kutoka Ufaransa na Uingereza.Marufuku hiyo ya Ujerumani ingekuwa ni mradi wa pamoja wa Ulaya kama ambavyo ilitokea katika Eurofighter au Tornado kama zilivyoitwa mjini Paris na London.Lakini vinginevyo inaonesha kwamba fedha ni muhimu zaidi kwa ulaya kuliko maadili.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Sekione Kitojo