Chama cha wafanyakazi Tunisia chaonya kuhusu demokrasia
24 Septemba 2021Katika taarifa yake uliyoitoa leo, muungano wa UGTT umeonya dhidi ya ukiritimba wake wa madaraka na kuhusu hatua yake ya kuifanyia mabadiliko katiba ya mwaka 2014. UGTT imesema inapinga hatua hiyo ya rais ya kufanya mageuzi na unaichukulia hatua hiyo kama hatari kwa demokrasia.
Kwa mujibu wa UGTT, ukiritimba huo unasababisha kuwepo mashaka kuhusu suala la kuwa na demokrasia imara ambalo Tunisia ilifanikiwa kudhibiti wakati wa vuguvugu la harakati za kudai mageuzi kwenye mataifa ya Kiarabu mwaka 2011.
Shughuli za bunge zimesitishwa
Julai 25, Rais Saied alimfuta kazi waziri mkuu, akasitisha shughuli za bunge na kuchukua madaraka kamili, hatua ambayo wapinzani wake wanaielezea kama mapinduzi. Siku ya Jumatano alikwenda mbali zaidi na kuifanyia mageuzi katiba ili kumruhusu kutawala kwa kutumia amri ya rais.
Muungano wa UGTT wenye wanachama milioni moja, ni muhusika muhimu katika siasa za Tunisia. Tayari ulishamuonya Rais Saied kwamba ingawa walipongeza hatua yake ya awali ya kuingilia kati mfumo wa kisiasa wa Tunisia uliokuwa umedhoofika, anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia katiba.
Vyama vikubwa vya siasa nchini Tunisia vimejitokeza kupinga hatua ya Saied, ambayo mkuu wa shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International Agnes Callamard, amesema leo kuwa unaweza kusababisha utawala wa kimabavu.
Spika wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi jana alitoa wito wa kuwepo harakati salama za kutafuta amani ili nchi hiyo isirejee kwenye utawala wa mtu mmoja, baada ya Rais Saied kutangaza kuwa ataongoza kwa kutumia amri ya rais.
''Mzozo ambao unatokea Tunisia hauhalalishi tu mapinduzi dhidi ya demokrasia. Unataka kuwepo mazungumzo ya taifa na mageuzi. Hali iliyopo leo ni hatari na mbaya zaidi kuliko iliyokuwepo kabla ya Julai 25,'' alifafanua Ghannouchi.
Vifungu vya katiba vyafutwa
Ghannouchi ambaye pia ni mkuu wa chama cha Ennahda, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba Rais Saied amevifuta zaidi ya vifungu 100 kutoka kwenye katiba. Amesema kiongozi huyo amechukua hatua hiyo kana kwamba Tunisia haina watu. Amewatolea wito wananchi wa Tunisia kuirejesha nchi hiyo kwenye njia ya demokrasia.
Baada ya rais kuchukua madaraka kamili, Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 80, aliweka kambi nje ya majengo ya bunge kwa muda wa saa 12. Huku Watunisia wengi wakiunga mkono hatua iliyochukuliwa na Rais Saied kutokana na kuchanganywa na mfumo wa kisiasa, baadhi ya wachambuzi wanasema hatua hiyo ni kikwazo cha demokrasia imara iliyoibuka nchini humo wakati wa vuguvugu la mwaka 2011 la harakati za kudai mageuzi kwenye nchi za Kiarabu.
(AFP, Reuters)