Chama cha ZANU-PF kimewafuta kazi wabunge 11 Zimbabwe
19 Januari 2018Chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF kimetangaza kuwafukuza ubunge, wabunge wake 11, washirika wa rais wazamani Robert Mugabe.
Haya yanajiri mnamo wakati rais Emerson Mnangagwa akiendelea kuchukua hatua dhidi ya wale waliokuwa wakimuunga mkono Mugabe pamoja na mkewe Grace. Mnangagwa alishika madaraka Novemba mwaka jana baada ya Robert Mugabe aliye na umri wa miaka 93 kulazimishwa kujiuzulu baada ya jeshi kuchukua mamlaka.
Naibu Spika katika bunge la Zimbabwe Mabel Chinomona amesema chama cha ZANU-PF kimeliarifu bunge kuwa wabunge hao kwa sasa hawawakilishi masilahi ya chama hicho. Baadhi ya wabunge waliokumbwa na hatua hiyo walikuwa ni mawaziri katika serikali iliyokuwa ya Mugabe.
Desemba mwaka jana chama cha ZANU PF kilitangaza kufuta uwakilishi wa wabunge watano washirika wa Mugabe akiwemo Jonathan Moyo mmoja wa wanasiasa waliokuwa katika kundi lillokuwa likimuunga mkono Grace Mugabe.