Chama tawala chashinda uchaguzi wa bunge Ethiopia
22 Juni 2026
Matokeo rasmi yaliyotangazwa jana Jumapili yameonesha kwamba katika uchaguzi huo uliofanyika Juni mosi wapiga kura walijitokeza kwa asilimia 94. Wapiga kura milioni 50 kati ya zaidi ya raia milioni 130 wa Ethiopia walijiandikisha kushiriki zoezi hilo.
Tume ya uchaguzi imesema mchakato huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa, hoja iliyoungwa mkono na Rais wa taifa hilo Taye Atske Selassie ambaye mara baada ya matokeo kutangazwa alisema kuwa, "Idadi ya waliojitokeza ni ya kipekee sana. Nimeshangazwa sana. Sikutarajia kwamba idadi ya waliojitokeza itazidi 94%."
Selassie aliongaza kuwa, iadi hiyo na mchakato wenyewe wa kupiga kura ni ushahidi kwa kila raia wa Ethiopia kwamba taifa hilo linapenda demokrasia amani, na maendeleo.
Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia, vituo 143 vya kupigia kura havikufunguliwa kutokana na ukosefu wa usalama katika majimbo ya Oromia na Amhara. Kwenye maeneo hayo, kuliripotiwa mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi ya wanamgambo hali iliyowazuia raia kushiriki kupiga kura.
Pia uchaguzi haukufanyika Tigray, ambako waratibu wammesema kulikuwa na mazingira yasiyofaa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili na mzozo wa kisiasa unaoendelea.
Ukosoaji mkali kwa mchakato mzima wa uchaguzi
Wachambuzi na wanasiasa wa upinzani wamekosoa vikali mazingira ya uchaguzi huo. Wamedai haukuwa huru wala wa haki na kwamba uligubikwa na hali ya hofu, vitisho, na ukandamizaji dhidi ya wapinzani.
Baadhi ya wakosoaji wakubwa wa serikali wamekuwa gerezani, uhamishoni au hawajulikani walipo, huku idadi kubwa ya wagombea wa upinzani wakizuiwa kushiriki.
Mmoja wa wagombea kutoka upande wa upinzani, Yitayal Assefa wa chama cha All Ethiopia Unity, ameeleza kuwa hakutarajia kushinda bali alishiriki ili kuwasilisha maoni yake kisiasa.
Kiongozi mwingine wa upinzani, Merara Gudina, aliyekataa kushiriki uchaguzi, amesema mchakato mzima ulikuwa wa udanganyifu na matokeo yake hayakushangaza.
Kwa mujibu wa tume ya chaguzi ya Ethiopia, bunge jipya linatarajiwa kuanza vikao vyake mwezi Oktoba, ambapo Abiy Ahmed anatazamiwa kuchaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Serikali yake inakabiliwa na makundi ya wanamgambo kwenye majimbo yake mawili makubwa ya Oromia na Amhara, kutokana na tofauti za kikabila na uwakilishi wa kisiasa.