1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Chama tawala nchini Senegal chadai kushinda uchaguzi

18 Novemba 2024

Chama tawala nchini Senegal cha Pastef, kimedai kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana Jumapili, na kufungua njia kwa chama hicho kutekeleza azma yake ya kuleta mabadiliko kwenye taifa hilo.

Uchaguzi nchini Senegal
Mmoja ya raia wa Senegal akipiga kura katika uchaguzi wa bunge uliofanyika Novemba 27 nchini SenegalPicha: John Wessels/AFP

Vyombo vya habari nchini humo vinaripoti kwamba chama hicho kinaelekea kupata viti 119 hadi 131 katika bunge la viti 165 kwa mujibu wa makadirio ya matokeo ya awali yanayojulikana hadi sasa.

Vyombo vya habari vinasema PASTEF kimepata ushindi kwenye matokeo ya vituo vingi vya uchaguzi ambako wametangaza matokeo yao ya awali, kikivishinda vyama vikuu viwili vya upinzani.  

Uchaguzi ulifanyika kwa amani nchi nzima ambako inaelezwa tayari asilimia 90 hadi 95 ya kura zimeshahesabiwa. Msemaji wa serikali Amadou Moustapha Ndieck Sarre amewashukuru wapiga kura kupitia kituo cha televisheni cha TFM akisema Wasenegal wamekipa ushindi mkubwa chama chake.

Rais Diomaye Faye alishinda uchaguzi wa rais mwezi March na aliahidi kuiletea Senegal mageuzi ya kiuchumi,kupambana na rushwa na kuleta mabadiliko katika masuala ya haki kwenye jamii.

Rais wa Senegal Diomaye Faye ndiye kiongozi wa chama cha Pastef Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Ahadi hii ndiyo iliyowapa matumaini wananchi na hasa miongoni mwa idadi kubwa ya vijana wa taifa hilo la Afrika Magharibi wanaokabiliana na mfumko wa bei na ukosefu wa ajira.

Lakini yote hayo alishindwa kuyatekeleza kutokana na bunge lililokuwa likiongozwa na upinzani kumzuia, hatua iliyomfanya rais Faye kulivunja na kuitisha uchaguzi huu wa mapema wa  bunge. Karine Bouaye ni miongoni mwa wapiga kura aliyetowa maoni yake baada ya uchaguzi.

"Bunge lililopita la 14  halikutufurahisha.Pengine bunge hili la sasa litakuwa bora, likiwa lina watu watakaokuwa bora kwa taifa letu''

Vyanzo mbali mbali vimeeleza kwamba idadi ya waliojitokeza kupiga kura jana Jumapili ilikuwa ndogo ikilinganishwa na iliyoshiriki uchaguzi wa rais.

Takriban Wasenegal milioni 7.3 walijiandikisha kupiga kura kuchagua watakaokalia viti 165 vya bunge la nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Rais wa zamani Makcy Sall anaongoza chama cha upinzani kinachoitwa Takku Wallu akiwa nje ya Senegal, na jana Jumapili chama hicho kilidai kwamba uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu na wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama tawala cha PASTEF, ingawa hakikutowa ufafanuzi wa madai yao.