1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Uingereza chakutana huku kikiwa na mgawanyiko

3 Oktoba 2017

Waziri Mkuu Theresa May ameeleza jitihada zake kuzikabili changamoto za kijamii na kutokana na ubaguzi wa rangi huku akitumai hilo litafanya watu kutotilia maanani migawanyiko kutokana na suala la BREXIT na uongozi wake.

Großbritannien Conservative Party - Parteitag in Manchester | Theresa May, Premierministerin
Picha: Reuters/H. McKay

Chama tawala cha kihafidhina nchini Uingereza kinafanya mkutano wake wa kwanza tangu kuchaguliwa tena mwezi Juni mwaka huu, lakini wanachama hawako katika hali ya kusherehekea. Waziri Mkuu Theresa May ameweka wazi jitihada zake kukabili changamoto za kijamii na kutokana na ubaguzi wa rangi huku akitumai hilo litafanya watu kutotilia maanani migawanyiko kutokana na suala la BREXIT na uongozi wake.

Udhibiti wa chama katika madaraka haupo imara, uungwaji wake mkono unazidi kuporomoka, na  serikali imezidi kugawanyika kufuatia Brexit. Kwa Waziri Mkuu Theresa May, mkutano huo wa kila mwaka ni fursa ya kukiimarisha au kukivunja chama na kuwazuia wanachama wanaojaribu kuchukua taji lake.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/H. McKay

Migawanyiko au fikra tofauti?

Bibi May anayetarajiwa kutoa hotuba yake siku ya Jumatano, katika mkutano huo unaofanyika Manchester, amesema yeye haweki mstari mwekundu kama wanavyofanya wengine au kama wanavyoutumia watu wengine msemo huo. Ameongeza kuwa"Kile ninachoweza kusema ni kuwa hakika ninafikiri uongozi ni kuhakikisha si kila mmoja katika timu yako anaitikia kila kitu, bali iwe timu yenye watu wenye fikra tofautitofauti ili kujadili masuala na kuafikiana na kuiweka mbele kauli ya serikali, na hilo ndilo tulilolifanya.”

May amesema ripoti ya uchunguzi inayoonesha namna watu wa rangi tofautitofauti huwajibikiwa katika sekta za afya, elimu, ajira na mahakama nchini Uingereza, itachapishwa tarehe 10.

Aidha mawaziri wake watatangaza sera za kuonesha serikali yake inafany akazi na kuonesha wakosoaji wa serikali yake wanapotosha.

Msimamo wa Boris Johnson

Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Reuters/H. Mckay

Lakini kwanza wajumbe wataisikiliza hotuba ya waziri wa Mambo ya nje Borris Johnson siku ya Jumanne. Johnson amelaumiwa kwa kumhujumu Waziri Mkuu huku akiiendeleza azma yake ya kuchukua uongozi kwa kutangaza mpango wake wa Uingereza kujiondoa rasmi kwenye Umoja wa Ulaya.

Huku mazungumzo ya Uingereza kujiondoa rasmi Umoja wa Ulaya yakiendelea kwa mwendo wa konokono, Johnson amejiweka kama anayetaka mtengano ulio safi lakini wenye masharti magumu. Miongoni mwa matakwa yake ni Uingereza kuchukua mfumo wa kodi za chini, kanuni ndogo za kudhibiti uchumi nje ya soko kuu la Umoja wa Ulaya na kwamba Uingereza haipaswi kulipa ili kufanya biashara.

Msimamo wa Johnson ambao una masharti magumu kuliko wa bibi May, umechangia hali ya hatima isiyotabirika kwa biashara za Uingereza.

Mwandishi: John Juma/APE/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW