Champions League-Bremen uwanjani.
22 Oktoba 2008Baada ya changamoto za jana za duru ya tatu ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya-mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich, mabingwa wa Ulaya Manchester United ma Arsenal na hata Juventus ya Itali zote zilikua na sababu ya kushangiria.
Leo duru hii ya tatu inaendelea kwa changamoto zaidi:Klabu ya pili ya ujerumani Werder Bremen ina miadi jioni hii na Panathaniakos katika kinyanganyiro cha kundi B wakati Sporting Lisbon wanacheza na Shakhtar Donetsk.
Werder Bremen ya Ujerumani ,inatumai jioni hii kutamba nyumbani mwa wagiriki Panathniakos na kuwaigiza wenzao Bayern munich walioizaba jana Fiorentina ya Itali mabao 3:0.Bayern munich lakini ilicheza jana nyumbani,Bremen iko ugenini kwa Panathniakos.Hatahivyo, inaahidi kila kitu chawezekana.Mpambano mwengine jioni hii kati ya Girondins Bordeaux ya Ufaransa na CFR Cluj na Sporting Lisbon na Donetsk.
Mashabiki lakini walisimkwa jana usiku pale mabingwa wa Ulaya manchester united walipowanyoa bila ya maji wenzao waskochi celtic kwa mabao 3:0.Mabao 2 ya mbulgaria Berbatov na moja la Wayne Rooney yalitosha kuzima vishindo vya mabingwa hao wa Scotland Celtic. Ushindi wa jana wa Manchester united umewapatia pointi 7 katika kundi lao E kufuatia mechi 3.Hivyo wako sawa na villareal ya Spain.
Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich,walisahau misukosuko yao ya karibuni na kutamba jana mbele ya wataliana Fiorentina kwa mabao 3:0.Miroslav klose alilifumania kwanza lango la Fiorentina dakika 4 tu baada ya kuanza mchezo.Halafu mwenzake Bastian Schweinsteiger akaupiga msumari wapili katika jeneza Fiorentina kabla mbrazil Ze Roberto kuwatia kaburini kwa bao lake la 3.
Olympique Lyon ya Ufaransa inaifuata Munich nafasi ya pili katika kundi hili ikiwa na pointi 5 .hii inafuatia ushindi wao wa mabao 5-3 dhidi ya steua Bukarest ya Rumania.
Arsenal London ikifuata nyayo za manchester iliitandika Fenerbahce ya Uturuki mabao 5-2 na hivyo, kusalia kileleni mwa kundi G.Hivyo, ni pointi 2 zaidi kuliko Dynamo Kiev ilioichapa FC porto bao 1-0 kutoklana na mkwaju wa freekick aliouchapa Alexander Aliev.
Juventus turin ya itali inashangiria ushindi mbele ya mabingwa mara kadhaa wa ulaya na spian Rela Madrid.Juventus ilitamba kwa mabao 2-1 baada ya del Piero kulifumania lango la Real kutokana na mkwaju wake kutoka masafa ya mita 25.Van Niestelrooy alifuta machozi ya Real kwa bao 1.
Nje ya champions League,AC milan ya Itali imethibitisha leo kwamba nahodha wa zamani wa Uingereza David Beckham atajiunga na klabu hiyo hapo Januari mwakani.Beckham anaeichezea wakati huu Los Angeles Galaxy baadae atarudi Los Angeles.
Mnamo miaka 2 iliopita FC Milan iliwafungisha mikataba mastadi kama Ronaldo na Ronaldinho wa Brazil,Shevchenko wa Ukraine na sasa David Beckham wa Uingereza.Beckham akiwa sasa na umri wa miaka 33 akionekana anaelekea kustaafu.