Champions League ; Fainali ya ndugu wawili wa mji mmoja
24 Mei 2014Hii ni fainali ya tano kuzikutanisha timu mbili za nchi moja katika Champions League barani Ulaya.
Pia timu zote hizo mbili zinawania kuufunga msimu huu kwa kunyakua mataji mawili wakati Real Madrid inawania kunyakua kombe hilo baada ya kuweka kibindoni kombe la mfalme, Copa del Rey, iwapo watanyakua kombe la Champions League, itakuwa ni mara ya kumi kwa klabu hiyo kuliweka katika jengo la klabu hiyo kombe hilo lenye hadhi ya juu katika bara la Ulaya ,na Atletico itakuwa ni mara yake ya kwanza kunyakua kombe hilo ikiwa ni wiki moja tu baada ya kutawazwa mabingwa wa ligi ya Uhispania , La Liga katika muda wa miaka 18.
Madrid ni tulivu
Mji wa Madrid uko baridi na mtulivu na matumaini badala ya hali ya wasi wasi imetanda na pia mji huo umegawika kabla ya fainali ya jioni ya leo Jumamosi baina ya mahasimu hao ambao ni watani wa jadi.
Tofauti na miji kama Glasgow, Roma na Buenos Aires , ambayo imegawanyika, na baadhi ya nyakati hutokea ghasia , kutokana na kandanda, uhasama na ushindani baina ya timu hizo mbili za mji wa Madrid kwa kawaida umekuwa wa amani na hata wa kirafiki. Uhasama mkali zaidi kwa Real Madrid ni dhidi ya Barcelona badala ya Atletico.
"Tusherehekee kwa amani " ni moja kati ya vichwa vya habari katika gazeti la michezo la AS siku ya Ijumaa.
Ndani ya habari hiyo, gazeti la michezo la AS limetoa maelezo ya mpambano kati ya Jose Luis Ramos, rais wa klabu ya mashabiki wa Real , na Julio de las Heras, rais wa Atletico Madrid.
"Kitu cha kwanza ambacho ningependa kukifanya ni kuwataka mashabiki wa timu zote mbili kuwa watulivu na amani, ili tuweke mfano duniani," amesema Ramos.
"Tumeona kile kilichotokea katika nchi kama Brazil, Argentina ama Italia.... Baba yangu alikuwa shabiki wa Real lakini pia alikwenda katika michezo ambayo Atletico inacheza. Amenifundisha kwamba kandanda sio vita," ameongeza.
De las Heras akajibu : "Nakubaliana na wewe kabisa , hususan kwa kuangalia kizazi cha vijana ambao wanapenda soka mno. Wanapaswa kuona kwamba mchezo wa mpira unapaswa kufurahiwa kwa amani."
Ramos amesema amefurahishwa mno na uwezekano wa Real kushinda taji lake la kumi la Champions League, wakati de las Heras amesisitiza kuwa "kile utakachoona badala yake ni taji letu la kwanza la Champions League.
Meya atoa wito wa utulivu
Meya wa mji wa Madrid, Ana Botella pia ametoa wito wa "amani na udugu" baina ya seti mbili za mashabiki.
Polisi wa mji huo tayari wameweka uzio wa waya kwa ajili ya usalama kuzunguka maeneo ya wazi ya Cibeles na Neptuno , ambako mashabiki wa Real na Atletico wanashangiria timu zao zinaposhinda.
Maeneo hayo mawili yanakaribiana mno lakini polisi wamesema hawatarajii matatizo makubwa, licha ya kuwa kiasi ya mashabiki 50,000 wanatarajiwa kumiminika katika kusherehekea katika moja ya maeneo hayo usiku kucha leo Jumamosi (24.05.2014).
Kiasi ya mashabiki 50,000 wa Atletico watafuatilia mpambano huo katika luninga kubwa katika uwanja wao wa Estadio Vicente Calderon. Baa na mikahawa pia imeweka televisheni kubwa.
Kiasi ya asilimia 70 ya wakaazi wa mjini Madrid wanatarajiwa kufuatilia mpambano huo wa fainali, ama nyumbani ama katika maeneo maalum ya wazi, pamoja na baa na mikahawa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Amina Abubakar