1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHAMPIONS LEAGUE-KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI ULAYA

26 Februari 2004
- JE,WABRAZIL AILTON NA DEDE WATACHUKUA URAIA WA QATAR-UARABUNI?
- NA WANARIADHA 2 WA KENYA HAWEZI KUIWALIOSHA BAHREIN


Ilikua wiki ya duru ya kwanza ya kutoana ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya-champions League.Mpambano wa kusisimua kabisa ulikua katika uwanja wa olimpik wa Munich kati ya mabingwa wa Ujerumani-Bayern Munich na mabingwa wa Spain Real Madrid.Mashabiki hasa wa Ujerumani walitaka kuwaona mastadi maarufu wa Real akina Ronaldo na Roberto Carlos wa Brazil,Zinedine Zedane wa Ufaransa,david Beckham wa Uingereza na Luis Figo wa Ureno na kwa kweli wote walikuwa uwanjani siku hiyo.

Lakini walikuwa mabingwa wa Ujerumani bayern munich waliotamba na kuhanikiza kwa mashambulio katika lango la Real.akina Beckham,Figo,Zedani na Ronaldo wote walitiwa mfukoni,hakuna aliefurukuta. Ilikuwa ni swali la wakati tu lini Munich ingetia bao.Michael Ballack na Roy Makay walikosea kidogo tu. Ze Roberto wa Brazil alitamba zaidi kati ya uwanja kuliko Zinedine Zedane, mchezaji bora wa dimba wa mwaka wa dunia.Roy Makaay alikua kitisho zaidi katika lango la Real kuliko Ronaldo.Na pale Makaay alipoipatia Munich bao la kichwa muda mfupi baada ya kukosea kidogo tu kutia bao pia kwa kichwa, ilikuwa wazi kwamba Munich ilistahiki ushindi.Lakini,kinyume na mkondo wa mchezo mnamo dakika ya 83 ya mchezo, Roberto carlos wa Brazil alichapa mkwaju mkali kutoka mita 35 ambao kipa wa timu ya Taifa na nahodha wa Bayern Munich,Oliver Kahn ulimtoka mikononi na kuteleza hadi wavuni mwa lango la Bayern Nunich.Hii ikawa kisa cha nahodha kuizamisha jahazi yake.Kahn alifanya vivyo hivyo katika kombe lililopita la dunia mjini Yokohama, Japan pale alipoutema mkwaju wa Rivaldo na hii ikampa nafasi ronaldo kutia bao la pili la Brazil na kutwaa Kombe la dunia. Kahn,ameahidi sasa kwamba atafuta madhambi yake hayo ya juzi pale Munich na Real zitakapokutana tena tarehe 10 Machi kwa duru ya pili lakini mjini Madrid.

Makamo-bingwa wa Ujerumani Stuttgart wamejichimbia jana kaburi wenyewe kwa mlinzi wao Fernando Meira kuunasa wavu wake mwenyewe mnamo dakika ya 12 ya mchezo wakati akijaribu kuokoa.sasa mambo yatakua magumu kwa Stuttgart kama vile yatakavyokua kwa weziwao mabingwa wa Ujerumani Bayern munich, watakaporudi uwanjani kwa duru ya pili ya kutoana.Munich ilimudu sare bao 1:1 na Real Madrid ya Spain hapo juzi baada ya kipa wao na nahodha wao Oliver kahn kuizamisha jahazi kwa kuachia mpira kumpenya hadi wavuni.Kahn ambae alishambuliwa mno na magazeti ya ujerumani wiki hii,ameahidi kwamba atafuta madhambi yake katika duru ijayo huko Madrid.

Chelsea walioshinda kila mpambano wa champions league nje ya Uingereza, walibidi kutoa shukurani kubwa kwa kipa wao Carlo Cudicini kwa kuzima hujuma za wastuttgart.Kipa huyo aliokoa mikwaju kutoka washambulizi wa Stuttgart Silvio meisner,Kevin Kuranyi na Alexander Gleb. Ama manchester united ya Uingereza itakuwa na kazi ngumu nyumbani kuzuwia isipigwe kumbo nje ya champions league b aada ya mabao 2 ya muafrika kusini Benni McCathy kuipatia FC porto ushindi wa mabao 2:1 la manchester.Bao la manchester lilitiwa na muafrika kusini mwengine anaetoka Cape town kama Mccathy: Quinton Fortune.Nahodha wa manchester Roy Keane alitolewa nje ya uwanja mnamo dakika ya 87 kwa kadi nyekundu . Ushindi wa porto pamoja na kuonywa kwa nahodha Roy Keane ,kutawasumbua sana Manchester duru ijayo na Porto inatuami kutetea ushindi wake wa jana.

Deportivo la Coruna ni timu pekee kati ya 4 za Spian zilizosalia mashindanoni ilioshinda katika duru hii ya kwanza ya kutoana ya kombe hili la Ulaya: Deportivo ilitoa Juventus ya Itali kwa bao 1:0. Real ilitoka suluhu na bayern munich 1:1. Taarifa kutoka Bremen zinasema mshambulizi wa Brazil Ailton anaeongoza orodha ya watiaji-magoli katika Bundesliga-Ligi ya ujerumani wakati huu anazingatia ombi la kumtaka abadili uraia na kuichezea Qatar ili kuisaidia kukata tiketi ya kombe lijalo la dunia hapa ujerumani. Mbrazil huyu aliekwishabandika mabao 19 hadi sasa hakuwahi kuitwa kuichezea Brazil. Desemba mwaka jana alielezea fikra hata ya kuchukua uraia wa ujerumani ili aichezee Ujerumani katika Kombe la dunia mwaka 2006.Kuhusu ombi kutoka Qatar,Ailton ameahdi kutoa tangazo juu ya uamuzi wake wiki ijayo. Kwa muujibu wa gazeti la BILD,Qatar itayari kumpa Ailton kitita cha dala milioni 1.2 kuichezea katika kuania tiketi za Kombe la dunia na kitita zaidi cha euro laki 4 akiamua kusalia Qatar.

Mbrazil mwengine Dede anaeichezea Borussia Dortmund pia katika Bundesliga ametakiwa na Qatar kuchukua uraia pamoja na nduguye Leandro.Dede ameungama kwamba kwa mwezi sasa amekuwa akiwasiliana na Qatar. Dede ametakiwa pia kuichezea timu ya taifa ya Qatar. Wabrazil 2 walikuwamo katika timu ya Tunisia iliotawazwa mabingwa wa Afrika kati ya mwezi huu huko Tunis. Wakati wabrazil wanashawishiwa kubadili uraia katika dimba na nchi za kiarabu, wakenya wanaipa mgongo bendera ya nchi yao katika medani ya riadha:hatahivyo, Leonard Macheru na Abel Cheruiyot waliochukua uraia wa Bahrein mwaka jana wamekataliwa ruhusa ya kukimbia kwa niaba ya nchi hiyo ya ghuba katika mashindano ya mwezi ujao ya ubingwa wa riadha wa dunia ukumbini-Indoor championship na katika mbio za nyika-cross-country za ubingwa wa dunia.

Shirikisho la riadha ulimwenguni IAAF limesema bingwa wa dunia wa masafa ya mita 3000 ukumbini-indoor- Mucheru anaeitwa sasa Mushir Salim na Cheruiyot-maarufu sasa kwa jina la Abel Yacoob Jowher salim hawataweza kukimbia chini ya Bendera ya B ahrein.Kwani Mucheru alishindana kwa jina la Kenya katika ubingwa wa nyika wa dunia mwaka 2003 huko Birmingham,Uingereza na Cheryot aliiwakilisha Kenya katika mbio za nyika za dunia mwaka 2002. Msemaji wa IAAF,Nick Davies akizungumza kati ya wiki hii mjini Monaco, amearifu wote wawili wangeweza kuiwakilisha bahrein baada ya kitambo cha miaka 3 kila mmoja tangu kubadili uraia.

Katibu wa chama cha riadha cha Kenya,david Okeyo amesema kuwa, Mucheru amechaguliwa na chama cha riadha cha Bahrein kukimbia katika mashindano ya mbio za nyika ya Machi 20 huko Ubelgiji.Mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia ukumbini-Indoor championships yataanza Machi 5 nchini Hungary. Wanariadha wengi wa Kenya wamekimbilia nchi za ghuba pamoja nao Stephen Cherono alieshinda ubingwa wa dunia wa mbio za masafa ya mita 3000 kuruka viunzi katika mashindano ya mwaka jana ya dunia mjini Paris alipokimbia chini ya bendera ya Qatar na kwa jina jipya la Saif Saeed Shaheen.Wanariadha wanaobadili uraia waweza tu kuziwakilisha nchi zao mpya baada ya kungoja kipindi cha mwaka tu ikiwa mashirikisho yote 2 ya riadha yataafikiana.Kenya ilikasirishwa mno pale Cherono alipowapokonya taji la mita 3000 kuruka viunzi mjini Paris mwaka jana, taji ambalo Kenya inadai ni mali yake na inashinda katika kila mashindano makuu.

Michezo ya Olimpik ya Athens, ikikaribia, mamia ya wagiriki walikusanyika kati ya wiki hii mjini Athens, mji mkuu na kituo cha michezo hiyo hapo August mwaka huu,kulalamika dhidi ya kufanyika michezo hiyo mjini humo. Kiasi cha wagiriki 5000 wengi wao vijana walishiriki katika maandamano ya amani .Wmelalamika kuwa usalama mkubwa uliowekwa kama vile makamera mamia kadhaa ya kuwakagua watu katika mji mzima wa Athens kunakiuka haki za uhuru wa raia.Haya ni malalamiko ya tatu mjini Athens, tangu januari.Waanfamanaji walipanga maandamano yao wakati mmoja na mkutano wa maafisa wa olimpik kutoka nchi 201 mjini Athens wanaokagua maandalio mbali mbali ya michezo hiyo ya olimpik ya mwaka huu, inayorejea katika nchi ya asili ya michezo hii. Maandamano mengine yamepangwa jumamosi siku ambayo wakuu wa IOC- halmashauri Kuu ya olimpik Ulimwenguni wanakutana mjini Athens.
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW