1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League kuanza rasmi Jumanne

20 Septemba 2013

Wachezaji Bayern Munich watakiwa kucheza kwa bidii zaidi,Dortmund yapata ushindi wa tano mfululizo katika ligi ya Ujerumani Bundesliga ,Ligi ya mabingwa, Champions League kuanza rasmi katika awamu ya makundi.

Katibu Mkuu wa UEFA Gianni Infantino wakati wa droo ya mechi za makundi za Champions League
Katibu Mkuu wa UEFA Gianni Infantino wakati wa droo ya mechi za makundi za Champions LeaguePicha: picture-alliance/dpa

Ulikuwa mchezo wa tano, na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Braunschweig ilikuwa haijapata points hata moja hadi jana. Kocha Torsten Lieberknecht alikuwa hashikiki, kwani kwa muda wa dakika 70 jana Jumapili(15.09.2013) timu yake ilikuwa tena nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Nuremberg.

Kikosi chake lakini kilikuwa kinaonesha dalili ya kupata ushindi licha ya kuwa nyuma, wakati baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakijiuliza iwapo timu hiyo haitaweza kupata ushindi dhidi ya Nuremberg ambayo nayo haijapata ushindi licha ya kuwa na sare tatu katika michezo minne, Braunschweig itapata ushindi dhidi ya timu gani.

Torsten Lieberknecht kocha wa BraunschweigPicha: picture-alliance/dpa

Ndipo Omar Alabdellaoui alipopachika bao la kusawazisha kwa Braunschweig mbele ya mashabiki wa nyumbani katika dakika ya 70 ya mchezo huo na kuamsha shagwe kubwa. Braunschweig imepata pointi yake ya kwanza katika Bundesliga msimu huu ambayo wameipata kwa kufanya kazi ya ziada, kama anavyoeleza mchezaji wa kiungo wa Braunschweig Karim Bellarabi.

"Katika dakika zote 90 tulijitahidi kuwa makini. Leo tuliweza kutumia uwezo wetu wote. Tunafarijika na kazi tuliyofanya. Ni bahati mbaya , kwamba leo hatukuweza kushinda. Tulikuwa timu bora . Ndio sababu tungeweza kupata ushindi, kwa ajili ya mashabiki wetu na kwa ajili ya mji wetu".

Borussia bado kiboko

Borussia Dortmund bado inaongoza ligi hiyo ikiwa imepata ushindi katika michezo yake yote mitano, na iliirarua Hamburg SV siku ya Jumamosi kwa mabao 6-2. Mshambuliaji Marco Reus wa Borussia amesema kuwa ulikuwa mchezo ambao unaleta raha.

"Hii ni dhahiri kuwa kila mara inaleta furaha, iwapo magoli yanapatikana. Hilo ndio kila mara la muhimu zaidi. Haina maana iwapo unacheza kama tulivyocheza na kisha hakuna magoli na mwishoni mnashindwa".

Marco ReusPicha: Reuters

Bayern Munich ilipata ushindi wa mabo 2-0 nyumbani dhidi ya Hannover 96 , lakini matokeo hayo hayakumfurahisha mkurugenzi wa spoti wa timu hiyo Matthias Sammer, ambaye amesema timu hiyo inapaswa kucheza kwa kujiamini zaidi pamoja na bidii katika mchezo wao.

Hata hivyo rais wa klabu hiyo Uli Honnes amejibu mapigo kwa kusema , timu hiyo hadi sasa haijapata kushindwa kwa hiyo hakuna sababu ya kulalamika. Amesema kocha Pep Guardiola ameingiza mambo mengi mapya katika kikosi hicho na anapaswa kupewa muda kuyaweka sawa.

Matthias Sammer mkurugenzi wa spoti wa BayernPicha: picture alliance/Sven Simon

Timu zote nne za Ujerumani ambazo zinashiriki katika kinyang'anyiro cha Champions League zimepata ushindi mwishoni mwa Juma. Bayer Leverkusen imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya VFL Wolfsburg, Schalke 04 ikaipiku Mainz 05 kwa bao 1-0.

Mchezaji ghali

Nchini Uhispania Gareth Bale ambaye amekuwa mchezaji ghali kabisa duniani kwa hivi sasa amepata bao lake la kwanza akivaa kwa mara ya kwanza jezi ya Real Madrid, katika mchezo ambao ulitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Villareal. Cristiano Ronaldo ameamua kujihusisha na klabu hiyo hadi mwaka 2018 akirefusha mkataba wake wa sasa na kuondoa uwezekano wa kuihama timu hiyo.

Nchini Uingereza mabingwa watetezi Manchester United ilifanyakazi ya ziada kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace , lakini Mesut Ozil aliwaonesha mashabiki wake kuwa anao uwezo wa kuibadilisha sura ya mchezo wa timu hiyo katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sundeland.

Cristiano Ronaldo wa Real MadridPicha: Getty Images

Matokeo mabaya hata hivyo yaliwaangukia vigogo Chelsea pale walipopata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Everton na Manchester City wakatoka sare ya bila kufungana na Stoke City.

Katika Champions League Bayern Munich inajaribu kwa mara ya kwanza kufanya kile kinachoonekana kuwa ni utetezi wa taji walilolipata msimu uliopita la Champions League na pia ni moja kati ya timu zilizopata makocha wapya msimu huu.

Guardiola yuko katika mbinyo

Pep Guardiola , ambaye aliiongoza Bacerlona kupata ushindi wa mataji mawili ya Champions League kati ya mwaka 2008 na 2012, amechukua mahali pa Jupp Heynckes ambaye amestaafu rasmi baada ya kuitawaza Bayern mabingwa wa mataji matatu katika msimu mmoja.

Mesut ÖzilPicha: picture-alliance/dpa

Guardiola anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuifanya timu hiyo kuwa timu isiyoshindika katika bara la Ulaya , ambayo mbali ya kupata ubingwa mwaka huu wa 2013, pia ilifikia fainali mwaka 2010 na 2012.

Mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge amesema kuwa klabu hiyo inalazimika kufanyakazi kuweza kujenga utamaduni wa kushinda taji hilo la Champions League mara kwa mara.

Guardiola hivi sasa yuko katika hatua za kukinoa kikosi hicho kiwe na makali ya kudumu kuliko pale kilipoinyoa Barcelona bila maji kwa kuichapa mabao 7-0 katika michezo miwili ya nusu fainali msimu uliopita na hatimaye kuishinda Borussia Dormund kwa mabao 2-1 katika fainali ya kwanza ya timu zote za Ujerumani katika fainali ya Champions League.

Champions League

Ujerumani itakuwa na timu nne katika kinyang'anyiro cha Champions League katika awamu ya makundi inayoanza kesho Jumanne kwa mara ya kwanza , na jibu la kwanza litapatikana mwishoni mwa mwaka huu wakati Bayern Munich , Borussia Dortmund , Bayer Leverkusen na Schalke 04 ambazo zote zinakwaana na timu kutoka Premier League zitakapoonesha matokeo yake.

Mlinzi wa zamani wa Leverpool Sami Hyypia anaoiongoza Bayer Leverkusen kesho katika kundi A ambapo inapambana na Manchester United, ambapo kocha wa zamani wa Everton David Moyes anafuata nyazo za Sir Alex Ferguson , ambaye aliiongoza timu hiyo katika mafanikio ya taji la Champions League mwaka 1999 na 2008.

Kocha wa FC Bayern Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa

Hyypia anadai kuwa haendi Old Traford kupata saini ya kumbukumbu ya Wayne Rooney , lakini kupata points za mwanzo katika kundi hilo ambalo pia lina timu za Real Sociadad na Shakhtar Donetsk.

Bayern inafungua kampeni yake ya kutetea taji lake na CSKA Moscow katika kundi D wakati Manchester City ambayo sasa inaongozwa na Manuel Pellegrini itakuwa katika jamhuri ya Czech kupambana na Viktoria Plzen.

Makamu bingwa Borussia Dortmund kabla ya kuchomoa upanga wake kupambana na Arsenal London , inakibarua na Napoli siku ya Jumatano, timu ambayo pia ina kocha mpya ambaye aliwahi kuzifunza Liverpool na Chelsea , Rafael Benitez na pia mshambuliaji mpya kwa jina la Gonzalo Higuain.

Arsenal inafungua dimba kwa kupambana na Olympique Marseille.

Schalke 04 iko katika kundi E pamoja na Chelsea ya Jose Mourinho ambapo timu hiyo ya Ujerumani inafungua dimba na Steaua Bucharest, wakati Chelsea inamiadi na Basel ya Uswisi.

"La Decima"

Vigogo vya soka nchini Uhispania , Real Madrid na Barcelona sio tu kwamba wana makocha wapya , lakini pia wamesajili wachezaji ghali kabisa msimu huu Gareth Bale na Neymar.

Kocha wa Bayer Leverkusen Sami HyypiäPicha: Picture-Alliance/dpa

Ushirikiano kati ya Ronaldo na Bale na Messi na Neymar utakuwa wa kuvutia machoni, wakati Real wanataka kwa udi na uvumba kupata taji lao la kumi, "La Decima", lakini matumizi ya zaidi ya euro milioni 600 katika misimu miwili iliyopita kununua wachezaji katika kikosi hicho yatakuwa kipimo iwapo hilo linaweza kutimia.

Bale amesema wakati akitambulishwa kwa klabu hiyo kuwa "Ninataka kuisaidia timu hii kupata "La Decima" , akimaanisha taji la kumi la Champions League kwa Real Madrid.

Real Madrid ina miadi na Galatasaray ya Uturuki kesho Jumanne katika kundi B ambalo pia lina timu za Juventus na Copenhagen. Barca ambayo inakumbana na AC Milan kwa mwaka wa tatu mfululizo iko katika kundi C, na ainaanza na Ajax Amsterdam.

Paris St Germain ambayo itacheza kesho Jumanne katika kundi C inapambana na Olympiacos.

Gareth BalePicha: Getty Images

Kombe la dunia

Na katika bara la Afrika michezo ya kuwania nafasi tano kwa timu za Afrika katika fainali za kombe la dunia mwakani itaanza rasmi mwezi Oktoba na timu kumi zilizofanikiwa kufikia katika awamu hiyo zimekwisha pangwa. Cote D'Ivoire inapambana na Senegal , wakati Cameroon imepangwa kuoneshana kazi na Tunisia. Ethiopia itacheza na Nigeria, wakati Ghana ina miadi na Misri. Burkina Faso ina kibarua dhidi ya Algeria.

Didier DrogbaPicha: picture-alliance/dpa

Mchezo kati ya Cote D'Ivoire dhidi ya Senegal ndio unaoleta hamasa zaidi kutokana na matukio ya hapo nyuma, baada ya Simba hao wa Teranga kupigwa marufuku kutumia uwanja wao mjini Dakar tangu pale yalipotokea machafuko na ghasia zilizosababisha mchezo huo kuvunjika wakati wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.

Mchezo huo ulivunjika dakika 14 kabla ya kumalizika baada ya mashabiki kufanya fujo ambapo Cote D'Ivoire ikiwa mbele kwa bao 1-0 kutokana na mkwaju wa penalti wa Didier Drogba na kuiweka Cote D'Ivoire katika udhibiti wa michezo yao hiyo miwili.

Wakati huo huo watu watatu wamejeruhiwa kwa risasi jana Jumapili mjini Nairobi wakati wa pambano la ligi kati ya Gor Mahia na Tusker, ambapo Tusker ilishinda kwa bao 1-0.

IOC

Rais mpya wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC, Thomas Bach ataingia katika ofisi yake mpya rasmi kesho Jumanne mjini Lausanne, nchini Uswisi , bila ya sherehe kubwa lakini akikabiliwa na mengi ya kufanya.

Rais wa IOC Thomas BachPicha: Getty Images

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 59, ambaye alichaguliwa Jumanne iliyopita mjini Buenos Aires , amemaliza sherehe za ushindi na sasa ni kazi.

Wakati changamoto kubwa ya Bach ni kuhakikisha michezo yenye mafanikio ya majira ya baridi mjini Sochi mwakani 2014 nchini Urusi ziara yake ya kwanza rasmi itakuwa mjini Olimpia nchini Ugiriki kuhudhuria uwashaji wa mwenge wa olimpiki. Amekwisha weka wazi malengo yake ya muda mrefu ya kipindi chake cha kwanza cha miaka minane katika hotuba yake ya ufunguzi.

Na kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kwa leo, jina langu ni Sekione Kitojo hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / rtre / ape / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW