Champions League makundi kupangwa leo
29 Agosti 2013Mshambuliaji maarufu wa klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo hatahudhuria upangaji leo wa makundi ya kinyang'anyiro cha Champions League mjini Monaco licha ya kuorodheshwa miongoni mwa wachezaji watatu ambao wanatarajia kupata tuzo ya mchezaji bora wa mwaka katika bara la Ulaya.
Mreno huyo ameorodheshwa pamoja na Lionel Messi wa timu hasimu ya Barcelona na Frank Ribery wa Bayern Munich mabingwa wa sasa wa champions League kuwa wagombea watatu wa tuzo hiyo, lakini badala yake ameamua kusafiri na timu yake ya Real Madrid kwenda katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Deportivo la Coruna.
Ronaldo anasemekana kuwa hakufurahishwa kwa kukiukwa mwaka jana wakati Andres Iniesta wa Barcelona alipotawazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo baada ya kuingoza Uhispania kufanikiwa kunyakua ubingwa wa mataifa ya Ulaya mwaka 2012.
Leo (29.08.2013)mjini Monaco kutafanyika sherehe hizo za UEFA pamoja na upangaji wa makundi ya timu katika kinyang'anyiro cha Champions League. Timu nne za Ujerumani zitashiriki, ikiwa ni pamoja na mabingwa wa Champions League Bayern Munich, makamu bingwa Borussia Dortmund, Bayer Leverkusen pamoja na Schalke 04.