1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHAMPIONS LEAGUE WIKI HII

Na Ramadhan Ali24 Februari 2005

CHAMPIONS LEAGUE-KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI ULAYA

-KENYA YAJIPATIA KOCHA MPYA KWA HARAMBEE STARS

-TANZANIA-MAKAMO-MWENYEKITI WA TFF KOROKORONI KWA KULA FEDHA ZA UMMA.

-EDITH MASDAI HATAIWAKILISHA KENYA KATIKA MBIO ZA NYIKA ULIMWENGUNI UFARANSA .

Bundesliga-Ligi ya Ujerumani ikiwa imerudi uwanjani jioni hii huku Bayern Munich na Schalke 04 zikikamatana koo pointi sawa kileleni,mashabiki wa Ulaya wanadurusu duru ya kati ya wiki hii ya Champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya.

Baada ya mapumziko ya majira ya baridi,Duru ya kutoana ya kombe hilo la Ulaya ilianza:

Viongozi wa Ligi ya Ujerumani-bayern munich walitamba mbele ya Arsenal London ya Uingereza.Real Madrid ilitamba mbele ya Juventus ya Itali na FC barcelona iliipiga kumbo Manchester united ya Uingereza.Tangu mabingwa wa Ujerumani Werder bremen hata ndugu zao Bayer Leverkusen walikiona kilichomtoa kanga manyoya.

Arsenal walijikuta wameshachapwa bao 1 na Bayern Munich zilipopita dakika 4 tu tangu kuanza mchezo.Muivory Coast Kolo Traore akijaribu kuokoa langoni mwa Arsenal aliutia kichwa mpira uliomuangukia Claudio Pizarro ambae aliutia kimiyani.Mperu huyo akasema-mramba asali-harambi mara moja. Kwani alirudi tena kuufumania mlango wa Arsenal kwa bao la pili mara tu baada ya kipindi cha mapumziko.Mwishoe, Mbosnia Hasan Salihamidzic akaupiga msumari wa mwisho katika jeneza la Arsenal katika Champions League.

Ikibainika kana kwamba, Arsenal imefarki dunia katika uwanja wa Munich, mlinzi wao aliewachimbia kaburi mjini Munich, Kolo Toure, aliifufua Arsenal kwa bao lake.

Kwa ushindi wa mabao 3:1 la Arsenal,Bayern Munich ina miadi nyengine na Arsenal hapo Machi 9 uwanjani Highbury,London kujaribu kuitia Arsenal kitanzi cha mwisho nje ya champions League.

Arsenal itakua na ajenda nyengine siku hiyo.Itahitaji kutia nta ngome yake isivuje kama ilivyovuja Munich na itie mabao 2 inayohitaji kufuta mabao 3:1 ya Munich katika duru ya kwanza.

Ama katika changamoto ya makipa wawili hasimu wanaoania nafasi ya kwanza katika lango la Ujerumani-kipa wa Bayern Munich Oliver Kahn na wa Arsenal-Jens Lehmann, kipa wa Arsenal mambo yalimuendea vibayxa siku hiyo.Kwani mabao 3 yalinasa wavuni mwake ingawa si kosa lake.Oliver Kahn aliachia bao 1 tu.

Kocha wa Ujerumani Jürgen Klinsmann aliekuwa uwanjani kuwaangalia wote 2, alitoa pongezi kwa wote na akasema ana bahati ya kuwa na makipa wawili maridadi kabisa.Atabidi hata hivyo kuamua ni yupi akae langoni mwakani wakati wa kombe la dunia.

Wakati Bayern Munich ilitamba dhidi ya Arsenal,Bayer Leverkusen ilikiona kilichomtoa kanga manyoya mbele ya FC Liverpool.Leverkusen ilizabwa mabao 3-1 na Liverpool.Ikicheza bila ya nahodha wake aliefungiwa kucheza Steven Gerrad,sasa iko njiani kuingia robo-finali ya kombe hili la klabu bingwa barani Ulaya.

Lakini kama Bayern Munich ilivyoregeza kamba dakika ya mwisho mbele ya Arsenal na kuachia bao,Liverpool imefanya madhambi kama hayo pale ilipomuachia Mbrazil Franca kuipatia Liverkuisen bao la matumaini.

Mabingwa mara kadhaa wa Ulaya-Real madrid waonesha wako njiani kutawazwa kwa mara ya 10 mabingwa wa Ulaya.Real iliizaba Juventus ya Itali bao 1:0.Kwa kweli ilistahiki ushindi mkuu mbele ya wataliana.

Hatima ya mabingwsa wa Ujerumani Werder Bremen katika Kombe hili natumai imeshakatwa,kwani Olympique Marseille ya Ufaransa ilithubutu kuikomea Bremen nyumbani mwao mabao 3:0.Mabao waliotia Sylvain Wiltord,Mahmadou Diarra na Juninho yalitosha kichimia Bremenkaburi nyumbani mwake.

Lyon iliowasili robo-finali ya Kombe hili msimu uliopita,sasa ina kila matumaini ya kucheza tena robo-finali,kwani kilichobakia ni kuwazika tu mabingwa wa Ujerumani hapo machi 8,nyumbani Ufaransa.

BARANI AFRIKA, Mahkama ya mjini Dar-es-salaam kati ya wiki hii ilimpa kifungo cha miaka 3 korokoroni makamo-rais wapili wa shiorikisho la dimba la Tanzania-bara (TFF) Bw.Aden Ismael Rage kwa madhambi ya kwiba dala 100,000.Hakimu Suma Seme alisema kwamba hii ni hatia mbaya kabisa ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Rage anatuhumiwa kwiba fedha hizo wakati akiwa Katibu-mkuu wa Shirikisho la dimba la Tanzania miaka 4 nyuma.

Kenya harambee Stars ilijipatia kati ya wiki hii kocha mpya-nae ni Mohammed Kheiri.Amechukua nafasi ilioachwa na kutimuliwa kwa Twahihir Muhiddin na wasaidizi wake 2.Inatokana na kushindwa kwa Kenya mabao 5-1 na Morocco mjini Rabat mapema mwezi huu katika kinyan'’aniyro cha kuania tiketi ya kombe la dunia kanda ya Afrika.

Kheiri anashika wadhifa wa ukocha wakati huu huku Shirikisho la dimba la Kenya likimsaka kocha barabara wa kigeni atakeiongoza Harambee Stars kwa muda mrefu.

Hii ni mara ya pili kwa Kheri mzaliwa wa Mombasa kushika hatamu za harambee Stars ,kwani ni yeye alieiongoza Kenya katika Kombe la Afrika la Mataifa nchini Algeria,1990.

Mwenyekiti wa chama cha mpira cha Kenya Bw.Alfred Sambu alinukuliwa kusema,

"Tumemchagua Mohammed Kheiri kutokana na maarifa yake makubwa katika dimba."

Mkutano uliomchagua Kheri ulihudhuriwa na wachezaji 20 wa taifa wa zamani na makocha ulitishwa mjini nairobi kumsaka kocha wa kujaza pengo la Muhiddin alietimuliwa pamoja na wasaidizi wake kufuatia kuzabwa Kenya mabao 5-1 na Morocco mjini Rabat,hapo Feburuari 9.

Kenya ina miadi kucheza na Botswana mjini Nairobi hapo machi 26.

Shirikisho la dimba la Morocco nalo liliahirisha kati ya wiki hii uamuzi wake iwapo kumripoti kipa mfaransa Fabien Barthez kwa shirikisho la dimba ulimwenguni-FIFA kwa kumtemea mate rifu wakati wa mechi ya kirafiki baina ya klabu yake ya Olympique Marseille na Waydad Casablanca ya Morocco.

Marseille ilimpiga faini kipa huyo baada ya jazba kupanda katika mechi hiyo na rifu kubidi kuisimamisha mnamo dakika ya 80 ya mchezo palipozuka ngumi uwanjani.Waydad casablanca ikiongoza wakati huo 2:1.

Endapo Shiorikisho la dimba la Morocco litamripoti Barthez kwa FIFA,anaweza akafungiwa kwa muda mrefu hatua ambayo yaweza kumaliza maisha yake ya dimba .

RIADHA NA MBIO ZA NYIKA ULIMWENGUNI:

Bingwa wa mbio za masafa mafupi za nyika ulimwenguni-Edith Masai ilibainika wiki hii kwamba hatagombea taji lake huko Ufaransa mwezi ujao.Masai mwenye umri wa miaka 37,aliumia goti wakati akifanya mazowezi mapema mwezi huu na kwahivyo hakuweza kushiriki katika mashindano ya kitaifa nchini Kenya.

kujitoa kwake katika mbio hizo kumechafua maandalio ya Kenya kwa mashindano hayo huko St.Etienne,Ufaransa kuanzia Machi 29-30.

Taji la dunia la edith Masai mwaka jana ndilo taji pekee Kenya ilishinda katika mashindano yasio ya timu mjini Brussels,Ubelgiji.

Wanariadha 5 wa Kenya miongoni mwao Eluid Kipchoge walikuwa hawakupiga hodi katika kambi ya maandalio huko Embu,chini ya mlima Kenya.Chama cha riadha cha Kenya kikarefusha muda wa mwisho wa kupiga kambi huko hadi jioni ya jumatano.,

Kinyan’ganyiro cha kuania wapi michezo ya Olimpik ya majira ya kiangazi 2012 kikihamia New York wiki hii,balozi wa zamani wa Marekani Richard Holbrooke alielezea matumaini mjini NY kuwa hisia dhidi ya Marekani zinazohusiana na uvamizi wake nchini Iraq pamoja na wasi wasi wa usalama kusidhuru nafasi za mji wa NY kuandaa Olimpik 2012.Holbrooke alietunga mapatano ya amani yaliomaliza vita vya Bosnia vilivyodumu kati ya 1992-95, aliwaambia maripota mjini NY kwamba wale ambao hawafurahishwi na siasa za George Bush,watambue kwamba ni mrithi wa kiti chake atakaekuwa Ikulu pale michezo hiyo itakapofanyika miaka 7 kutoka sasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW