Champions League yarejea uwanjani
12 Februari 2018Ligi ya mabingwa barani Ulaya inarejea uwanjani kesho Jumanne, ambapo michezo miwili itarindima uwanjani na kisha keshokutwa Jumatano viwanja viwili tena vinatarajiwa kuwaka moto.
Mabingwa mara mbili wa taji hilo la Champions League barani Ulaya Juventus Turin wataoneshana kazi kesho Jumanne na timu inayoonesha kung'ara katika Premier League ya England Tottenham Hot Spurs katika pambano lao la kwanza katika kinyang'anyiro hicho. Washambuliaji hatari Harry Kane wa Spurs na Gonzalo Higuain wa Juve watakuwa kivutio kikubwa katika pambano hilo la timu 16 zilizobakia katika kinyang'anyiro hicho.
Manchester City ambayo ina paa katika Premier League ya England nayo inafunga safari kwenda mjini Basel kutiana kifuani na kikosi cha Basel ya Uswisi. Siku ya Jumatano itakuwa zamu ya FC Porto ya Ureno ikiikaribisha Liverpool ya Uingereza pia , na siku hiyo hiyo itakuwa lile pambano baina ya misumeno mikali ya kukata minyororo wa ulinzi. Real Madrid itaikaribisha Paris Saint Germain ya Ufaransa. Cristiano Ronald akiongoza kundi la washambuliaji Kareem Benzema na Gareth Bale , wakati Neymar ataliongoza kundi la kina Kylian Mbappe na Edinson Cavanni.
Jumanne ijayo shughuli itahamia mjini London ambapo Chelsea itaikaribisha FC Barcelona na Bayern ya Ujerumani inaikaribisha Besiktas ya Uturuki na siku inayofuata Jumatano FC Sevilla itapimana nguvu na Manchester United , na Schaktar Donezk ya Ukraine itaikaribisha AS Roma ya Italia.
Barani Afrika
Na katika bara la Afrika michuano ya awali ya kombe la Champions League ilifanyika mwishoni mwa juma, ambapo nchini Nigeria timu ngeni katika kinyang'anyiro hicho Plateau United iliishinda bila taabu na Mountain of Fire , Mlima wa Moto MFM ikitoka sare ugenini. Plateau ikiishinda Eding Sport wa Cameroon kwa mabao 3-0 na MFM ilitoka sare ya bao 1-1 na Real Bamako ya Mali.
Kiungo mchezeshaji wa Manchester City Kevin De Bruyne anaweza kuwa mmoja kati ya wachezaji watakaowania kwa karibu tuzo ya mpira wa dhahabu Ballon d'Or iwapo timu hiyo itashinda mataji makubwa, kwa mujibu wa kocha wake Pep Guardiola. De Bruyne amekuwa muhimu katika msimu huu ambapo City imekuwa ikitawala ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 akitoa usaidizi wa kufunga mabao mara 14 ikiwa ni kiwango cha juu katika ligi hiyo ikiwa ni pamoja kutoa usaidizi wa mabao 3 katika kipingo walichoiangushia Leicester City cha mabao 5-1 mwishoni mwa juma.
Nae kocha wa Liverpool Juergen Klopp amemmwagia sifa mlinzi Virgil van Dijk kwa utulivu aliokuwa nao katika pambano la jana Jumapili ambapo Liverpool iliishinda Southampton kwa mabao 2-0 wakati mdachi huyo aliporejea kwa mara ya kwanza kwa mwajiri wake wa zamani kabla ya kuhamia Liverpool.
Kocha wa Leicester City Claude Puel anaamini mgomo wa siku 10 wa winga machachari Riyad Mahrez ilikuwa ni kosa na ana matumaini kwamba kila mmoja atajitoa kutoka katika tukio hilo na kusonga mbele. Mahrez alirejea kufanya tena mazowezi na timu hiyo siku ya Ijumaa kwa mara ya kwanza tangu pale alipotoa ombi la kutaka kuihama timu hiyo mwezi uliopita huku vyombo vya habari vikisema mchezaji huyo amefadhaika sana baada ya kushindwa kuhamia Manchester City.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef