Champions League
16 Septemba 2010Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich walisubiri hadi dakika za mwisho kuwanyamazisha AS Roma 2-0 ilhali Chelsea na Arsenal walikuwa na kibarua rahisi, pale mechi za makundi za kombe la Klabu bingwa barani Ulaya zilipoingia siku yake ya pili jana usiku.
Jose Mourinho ambaye alishinda kombe la Champions League na Inter Milan msimu uliopita katika uwanja wa Santiago Bernabeu, jana alianza vyema na timu yake mpya ya Real Madrid- bao la beki wa Ajax Anita Vurnon lilipowapa Madrid bao lao la kwanza kabla ya Muargentina Gonzalo Higuain kuwahakikishia Real Madrid ushindi wa mabao 2-0 katika kundi la G.
Lakini Kocha wa Ajax Martin Jol anaamini utaalamu na ujuzi wa Real Madrid ndio ulikuwa muamuzi.
'' Ilikuwa ni kama mechi kati ya wanaume na chipukizi.'' Alisema Jol.
'' Tulicheza vizuri sana, na tulihakikisha Ajax, hawachezi mchezo wao.'' Ndio ilikuwa majibu ya Mourinho ambaye kwanza alihamakishwa na jinsi wachezaji wa Real Madrid, mfano Christiano Ronaldo walivyopoteza nafasi nyingi.
Zlatan Ibrahimoviv ndiye alikuwa muokozi wa AC Milan, wapinzani wakuu wa Real Madrid katika kundi la G alipotingisha wavu la Auxerre mara mbili na kuwapa AC Milan ushindi wa mabao 2-0.
Uwanja wa Allianz Arena ulikuwa kimya hadi dakika ya 79 pale Thomas Mueller alipoifungia Bayern Munich bao la kwanza dhidi ya AS Roma, dakika nne baadaye mkwaju wa Miroslav Klose ukawanyamazisha kabisa Waitaliano.
Uwanjani Emirates- Arsenal waliwaadhibu Braga ya Ureno mabao 6-0 katika mechi kocha wa Braga alisema alitamani mchezo ungefutiliwa mbali baada ya kipindi cha kwanza.
Cesc Fabregas ambaye alionekana amesahau ile hamu yake ya kuihama Arsenal kwenda Barcelona alitingisha wavu mara mbili, kabla ya Maroune Chamakh, Mrusi Arshavin na Carlos Vela kuwatumia salamu Braga wanaocheza katika Ligi hii ya Champions League kwa mara ya kwanza, kwamba wana kibarua cha ziada.
'' Tulicheza vibaya sana, nilitamani mechi yenyewe ingemalizika katika kipindi cha kwanza, na hata hivyo pia tulikuwa tumelemewa sana.'' Alisema kocha wa Braga Domingos Paciencia baada ya mechi hiyo.
Nicholas Anelka alifunga mabao mawili alipoingoza Chelsea iliyokuwa na kibarua rahisi mbele ya Zilina ya Slovakia kwa mabao 4-1 katika kundi la F. Spartak Moscow ya Urusi iliinyamazisha Olympique Marseille kwa bao moja kwa bila pia katika kundi hilo la F.
Mwandishi: Munira Muhammad/RTRE
Mhariri: Othman Miraji