1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League,kisa cha Armstrong na Kenya na Shirikisho la kandanda-FIFA.

26 Agosti 2005

Mabingwa Bayern Munich,wameanza vyema msimu huu kutetea taji lao,lakini pia Schalke makamo-bingwa na halkadhalika,Werder Bremen na FC Cologne.Jioni hii Cologne, iliopanda tena daraja ya kwanza kutoka ya pili, ina miadi nyumbani na Kaiserslauten.Cologne, iliotolewa jumamosi iliopita katika Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani na kikckers Offemnbach, iliwasangaza mashabiki na mahasimu ilipoizaba Stuttgart kwao mabao 3-2 na kutoroka na pointi tatu.Leo, wanacheza nyumbani .

Mabingwa Bayern Munich wako pia uwanjani katika Allianz Arena, uwanja wao mpya na maridadi wakiwakaribisha Hertha Berlin.

Eintracht Frankfurt timu nyengine iliopanda daraja ya kwanza kutoka ya pili msimu huu, iko nyumbani ikicheza na Nüremberg.Hamburg SV ambayo kati ya wiki hii ilikata tiketi yake ya Kombe la UEFA-Kombe la shirikisho la dimba la Ulaya baada ya kuitoa valencia ya Spain,ina miadi na jirani zao wa kaskazini Hannover.Schalke makamo-bingwa ambao kama Bayern Munich na Bremen wamekata tiketi za champions League ,wanakutana na Borussia Moenchengladbach.Wolfsburg wana miadi na Bayer Leverkusen wakati Bremen leo inakamilisha agenda na Stuttgart.

Kesho mapambano 2 yatakamilisha duru hii ya BUNDESLIGA:Arminia Bielefeld itacheza na Mainz na MSV Duisburg itachuana na B.Dortmund.

CHAMPIONS LEAGUE:

Firimbi ililia kati ya wiki hii kuanzisha msimu mpya wa Champions League:Mabingwa watetezi FC Liverpool ya Uingereza, wana miadi na mabingwa wa Premier League- Chelsea katika duru za kwanza za makundi.Haya yatakua marudio ya nusu-finali ya mwaka jana pale Liverpool ilipoitoa Chelsea.Anderlecht ya Ubelgiji itaania uongozi wa kundi G na Real Betis ya Spain.Kura ya alhamisi imezikutanisha tena timu mbili nyengine zilizokumbana katika nusu-finali AC Milan ya Itali na PSV Eindhoven ya Uholanzi.Timu hizo mbili ziko kundi moja na schalke ya Ujerumani na Fenebahce ya Uturuki inayoongizwa na kocha Christopher Daum.

Mabingwa mara 9 wa Kombe la ulaya-Real madrid ya Spain , imeangukia kundi moja na mabingwa wa Ufaransa Olympique Lyon.Timu nyengine katika kundi hili ni Olympiakos Piraeus na Rosenborg trondheim huku mabingwa wa Spain FC Barcelona ,wataridhika kukutanishwa na Panathniakos,Werder Bremen na Udinese.

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich na Juventus ya Itali zote mabingwa nyumbani, wanakutana tena katika kundi A na wanatumai kusonga mbele pamoja kwa kuzitoa mhanga Bruges ya Ubelgiji na Rapid Vienna ya Austria.

Manchester United ya Uingereza ,ikicheza kwa mara ya 10 katika hatua hii ya duru za kwanza za makundi, ina miadi na chipukizi wa kombe hili Villarreal,Lille na mabingwa wa zamani wa Ureno wa enzi za Eusebio-benefica Lisbon.AC Milan inarejea Istanbul,Uturuki uwanja wa finali walimoshindwa na mabingwa FC Liverpool.Miadi yao ya kwanza itakua na Fenerbahce.

Ama barani Afrika, FIFA-shirikisho la dimba la ulimwenguni,limevitaka vikundi 2 vinavyoania madaraka ndani ya chama cha mpira cha Kenya KFF kumaliza haraka ugomvi wao ambao wiki iliopita ulizusha machafuko.Makamo Katibu mkuu wa FIFA Jerome Champagne ametaka kikao kinachokuja cha halmashauri ya KFF kiahirishwe na kwamba FIFA, haitatambua maamuzi yoyote yatakayokatwa kutoka kikao hicho ikiwa hakitafutwa.FIFA imependekeza maamuzi yote kuhusu siku za usoni za chama cha mpira cha Kenya KFF yaahirishwe hadi mwisho wa mwaka huu.Kwa wakati huu, FIFA imependekeza Kenya kujishughulisha na mchezo wa dimba badala ya kinyan’ganyiro cha madaraka katika uongozi.

Barua ya makamo katibu mkuu wa FIFA ilifuatia kuhujumiwa kwa wauu 2 wa KFF na gengi la vijana wanaosemekena wanaelemea upande wa kundi moja kati ya hayo 2 yanayovutana pamoja na ajali ya gari ya kutatanisha iliozuka kati ya wiki.Ajali hiyo ilimjeruhi vibaya mwenyekiti wa KFF Alfred Sambu.

Amri ya FIFA imetoka huku hofu zikiwepo kuwa hali nyeti ya hivi sasa yaweza ikaharibika mno kuanza mwishoni mwa wiki hii msimu mpya wa Ligi ya Kenya pamoja na kikao maalumu cha KFF kilichoitishwa kutatua mzozo huu.

Uamuzi uliotolewa na FIFA unaitumbukiza moja kwa moja katika ugomvi huu na seriali ya Kenya iliosema kikao cha leo jumamosi cha shirikisho la dimba la kenya kisonge mbele kufanyika.

Waziri wa michezo wa Kenya Ochilo Ayacko alisema hapo awali alielewa kuna baadhi ya watu waliopanga kuuchafua mutano huo .

LANCE AMSTRONG BINGWA WA MBIO ZA BAISKELI MRA 7 ZA TOUR DE FRANCE :

Muamerika Lance Arsmstrong aliendelea mfululizo wiki hii kukanusha ripoti za gazeti la Ufaransa L’Equipe kuwa akitumia madama ili kuimarisha misuli (EPO).

Mkurugenzi-tendaji wa mbio za baiskeli za Tour de France-Jean-Marie Leblanc alisema amehisi amevunjwa moyo na Armstrong kufuatia mashtaka ya gazeti la L’equipe kuwa 1999- mwaka wa kwanza aliposhinda mbio hizo alitumia madawa .

Armstrong aliwahi kuugua maradhi ya Kensa na kupona. Aliibuka bingwa mkubwa kabisa wa mbio hizo za Tour de France.Binafsi ,anatesa,”Nitakariri tena na tena sikuwahi kutumia madawa ya kutunisha misuli.”

TUMALIZIE NA MBIO ZA MAGARI AMBAMO HATIMA YA BINGWA MWENGINE MAARUFU IMO MASHAKANI:Kampuni la magari la FERRARI huko Itali lasemekana halitarefusha mkataba wa bingwa mara 7 Michael Schumacher pale utakapomalizika mwishoni mwa mwaka ujao wa 2006.Mahala pake ,Ferrari inapanga pachukuliwe na Kimi

Raikkonen wa Finland.Hii ni kwa muujibu wa gazeti la BILd la Ujerumani litokalo kila siku.Schumacher alishinda mara 5 mfululizo akiendesha Ferrari,lakini gari za Ferrari msimu huu hazikufua dafu mbele ya Renault na McLaren-Mercedes ambazo ndizo zilizo tia fora.Gazeti la Bild limearifu kwamba ,Schumacher atajiunga na McLaren-Mercedes mkataba wake utakapomalizika.

Raikkonen ameshinda mbio 5 msimu huu kwa motokaa za McLaren na yuko nafasi ya pili katika orodha ya madereva wanaoania ubingwa wa dunia nyuma ya Fernando Alonso anaendesha gari la Renault.Schumacher ameangukia nafasi ya tatu nyuma yao.Gazeti la BILd limearifu kuwa, Raikkonen na Ferrari wametiliana saini ya kwanza hapo mwezi Mei.

Gazeti la BILD linadai taarifa zake ni siri ya mtungini kutoka duru ya kuaminika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW