1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions Ligi yaanza kutimua vumbi

Sekione Kitojo
12 Septemba 2017

Michuano ya vilabu barani Ulaya ya Champions League inaanza rasmi msimu huu leo Jumanne(12.09.2017), ambapo timu 16 zitaingia uwanjani jioni hii , kuwania pointi  muhimu kujiweka vizuri kuingia katika duru ya mtoano.

Fußball TSG 1899 Hoffenheim v FC Bayern München - Bundesliga
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ujerumani  inawakilishwa  na  timu  tatu , Bayern Munich , Borussia Dortmund  pamoja  na wageni katika  ligi  hiyo RB Leipzig.

Bayern Munich  inajitupa  katika  uwanja  wa  Allianz Arena  mjini Munich  wakiwakaribisha  Anderlecht  ya  Ubelgiji, jaribio  ambalo halitakuwa  na  changamoto  kubwa  kwa  kikosi  hicho  cha  kocha Carlo  Anceloti. Hali  ya  katika  klabu  hiyo  kwasasa  ni  ya mawimbi, kutokana  na  matamshi  ya  mshambuliaji  wa  kutumainiwa wa  klabu  hiyo  Thomas Muller  kwamba  kuna  maisha  hata  bila Bayern  Munich yanaleta  hali  ya  shaka shaka  kwamba  mchezaji huyo  ana  nia  ya  kuihama  Bayern  pengine  msimu  ujao, kutokana na  kutopata  nafasi  ya  kucheza  kila  mara  katika  kikosi  cha Anceloti.

Mchezaji Thomas Mueller wa Bayern MunichPicha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Hata  mshambuliaji  mahiri  wa  Bayern Munich Robert Lewandowski ametumbukia  katika mjadala  mkubwa  hapa  Ujerumani  baada  ya kuikosoa sera  ya  klabu  hiyo ya manunuzi  ya  wachezaji  wapya. Lewandowski  amekosoa  sera  hizo  na  kusema , klabu  hiyo haijaweza  hata  kuvuka  kiwango  cha  euro milioni 40  kununu wachezaji  wapya  na  hali  hiyo  itaiacha  klabu  hiyo  nyuma ikilinganishwa  na  vilabu  kama  Paris St. Germain, Barcelona, Real Madrid, Manchester  United  na  vingine.

Lakini wachezaji  hao  wametakiwa  kucheza  kandanda  katika klabu  yao  na  sio  kuropoka. Ni  swali  la  kungoja  na  kuona  iwapo Bayern itashinda  kwa  kishindo  leo  dhidi  ya  Anderlecht  ndipo itakapoonekana  iwapo  kibarua  cha  Carlo Ancheloti  haitaota majani.

Kocha wa Bayern Munich Carlo AncelotiPicha: Imago/Thomas Frey

Barca inajaribu tena

Fainali  ya  Champions League  ya  mwaka  2015 kati  ya  Barcelona na  Juventus Turin  ambapo , Barca  waliirarua Juve  kwa  mabao 3-1 itakumbukwa  tena  leo  jioni  wakati  timu  hizo  zitakapokipiga katika  uwanja  wa  Camp Nou.  Pambano  la  mwaka  jana  la  robo fainali  ambapo  Juve iliibuka  kidedea bado liko katika  hisia  za wachezaji  na  mashabiki  wa  Barcelona.

Manchester  United  imerejea  katika  makaazi  yake  ya  kawaida katika  Champions League  na  inakabiliana  na  timu  bora  kabisa katika  bara  la  Ulaya. Man U imeshindwa  kufuzu  kucheza  katika Champions League mwanzoni  mwa  kampeni  ya  kwanza kocha nyota Jose  Mourinho  alipochukua  uongozi  wa  kikosi  hicho  lakini ushindi  wao  wa  kombe  la  Ulaya  msimu  uliopita  ulitosha  kutoa ishara  ya  mambo  yajayo. Man U inakumbana  na  basel  ya  uswisi jioni  ya  leo.

Kikosi cha BarcelonaPicha: picture-alliance/Actionplus

Michezo  mingine  ni  kati  ya  AS Roma  ikiikaribisha Atletico  Madrid , timu  iliyonusa fainali mara  mbili  dhidi  ya  Real Madrid  na kushindwa  katika  muda  wa  miaka  mitatu  iliyopita. Chelsea inaikaribisha Qarabag timu  ambayo  nayo ndio kwanza  inaonja hewa  katika  anga  hilo  la  juu kutoka  Azerbaijan. Benfica ya Ureno inaikaribisha  ZSKA Moscow , na Olympiakos ya Ugiriki  ni  wenyeji wa Sporting Lisbon.

Macho yote kwa PSG

Lakini  macho ya  mashabiki  yataelekezwa  zaidi katika  mtanange baina  ya  Celtic  wakiwa  wenyeji  wa  Paris St. Germain. Mchezo huo utavutia  hisia  za mashabiki kwa  kutaka  kuwaona Neymar ambaye  hivi  karibuni  alikuwa  katika  kila  chombo  cha  habari baada  ya  kuitupa  mkono  FC Barcelona  na  kujiunga  na  timu hiyo iliyonununuliwa  na  kampuni  ya  uwekezaji  wa  Qatar. Mapambano  yanaendelea  hapo kesho kwa  kundi  jingine  la  timu 16  kupambana. RB Leipzig inaikaribisha  AS Monaco ya Ufaransa, wakati Borussia  Dortmund  itakuwa mjini  London katika  uwanja maarufu  wa  Wembley wakipambana  na  Tottenham Hot Spurs. Kila la  kheri.

Mchezaji wa PSG NeymarPicha: picture-alliancedpa/AP/K. Zihnioglu

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe /rtre /dpae

Mhariri: Yusuf , Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW