1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Changamoto mpya kwa wakimbizi wa Sudan nchini Chad

9 Julai 2024

Maelfu ya watu wanaokimbia mapigano nchini Sudan wanakabiliwa na changamoto mpya katika nchi jirani ya Chad. Miongoni mwa changamoto hizo ni njaa, magonjwa na makundi ya kutoa misaada yamesema yamelemewa na hali.

Sudan I Wakimbizi wakiwa kambini
Wakimbizi wa Sudan wakiwa kwenye moja ya kambi ya wakimbizi.Picha: Florian Gaertner/IMAGO

Katika mji wa Mashariki mwa Chad wa Adre, wakimbizi wanaendelea kumiminika huko kwa usafiri wa punda na wengine hata kwa miguu. Mji huo ukiwa mpakani mwa Chad na Sudan, upo katika hatari ya kutokea mgogoro wakati maelfu ya wakimbizi wa Sudan wakielezea namna wanavyokabiliana na maisha magumu, baada ya kutoroka vita nchini mwao.

Kwa miezi 15 sasa Sudan imeshuhudia vita vikali kati ya vikosi vya kiongozi wa jeshi wa taifa hilo Jenerali Abdel Fattah Al Burhan na Kiongozi wa wanamgambo wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, hali iliyopelekea maelfu ya watu kukimbilia katika nchi jirani ikiwemo Chad.

Taifa hilo linawahifadhi wakimbizi zaidi ya milioni moja hii ikiwa ni kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR. Thuluthi tatu kati yao, wameyatoroka mapigano katika mataifa yaliyo jirani na Chad kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon na Sudan.

Soma pia:Vita na uporaji vyaripotiwa katikati mwa Sudan

Shirika la Misaada ya Kiutu la Umoja wa Mataifa OCHA limeripoti kwamba ndani ya miezi mitatu iliyopita, watu 143,000 wamepoteza makaazi yao katika eneo la El Fasher nchini Sudan lililopo Kaskazini mwa mji wa Darfur.

Hili ni ongezeko la asilimia 15 la wakimbizi, hali inayoongeza kibarua kikubwa juu ya kile kilichopo cha kuwashughulikia wakimbizi waliopo.

"Hatuna kitu cha kula, tumeacha kila kitu nyuma, sijui nitafanyaje hapa bila kitu chochote." Alisema.

"Niliondoka El Fasher wiki moja iliyopita na watoto wangu watatu. Tumekaa siku kadhaa njiani bila chakula. Mtoto wangu mmoja akaaga dunia. Nimefika hapa na watoto wawili ambao sasa ni wagonjwa," alisema Mediha Zenaba Abdoulaye mkimbizi anaeomba msaada kwa familia yake.

Hali ya Wakimbizi nchini Chad

Abdoulaye kama wenzake wengine, safari yake ndio mwanzo imeanza, yeye na familia yake wapo nyuma kabisa ya msitari wa kupokea msaada, wale waliokuja mbele yake pia wapo katika msururu huo mrefu wa kusubiri msaada wa chakulana makazi, na bado kuna wimbi jengine kubwa linaloingia nchini humo.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

01:16

This browser does not support the video element.

Patric Youseff mkurugenzi Mkuu wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ICRC barani Afrika, ameiambia DW kwamba wanahitaji msaada zaidi kwasababu changamoto ni kubwa. Idadi kubwa ya wakimbizi inatarajiwa kuingia Chad iwapo eneo la El Fasher litaangukia mikononi mwa wanamgambo wa RSF

Dr Dieudonne Kouamegni ni moja wa madaktari wanaofanya kazi na shirika la madaktari wasio na mipaka MSF mjini Adre. Amesema visa vingi vya utapia mlo wanavyovishuhudia hasa miongoni mwa watoto wa wakimbizi kuna mengi wataalamu hao wa afya wanaweza kufanya kuboresha maisha ya watoto hao. 

Soma pia:UN: Nusu ya raia wa Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Kouamegni amesema wamepata wagonjwa 3000 ndani ya miezi mitatu iliyopita, 1,200 wamelazwa na miongoni mwa idadi hiyo asilimia 45 wanaugua utapia mlo na asilimia 32 ni magonjwa ya watoto.

Jerome Fritsch ni miongoni mwa madaktari wa watoto anasema kuna haja ya usaidizi zaidi wa chakula katika eneo hilo.

Ongezeko la wakimbizi nchini Chad pia kunatoa changamoto kubwa kwa uchumi wa taifa hilo, bei ya bidhaa imeongezeka na kufanya gharama ya maisha kupanda sio tu kwa wakimbizi lakini pia kwa raia wa taifa hilo.

Changamoto nyengine ni unyanyasaji wa kingono unaowakumba wanawake na wasichana kukiwa na wito wa kuwalinda  na kuwaunga mkono waathiriwa hao. Visa hivyo vinadaiwa kufanywa na vikosi vya jeshi katika maeneo ya vita.