1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za kuunda serikali ya muungano Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
27 Septemba 2017

Kiwingu kimetanda katika juhudi za kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne, CDU, CSU, FDP na die Grüne, unaojulikana kama Jamaica kutokana na rangi za vyama hivyo

Deutschland Bundestagswahl Merkel PK
Picha: Reuters/F. Bensch

Kiwingu kimetanda katika juhudi za kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne, CDU, CSU, FDP na die Grüne, muungano unaojulikana kama "Jamaica" kutokana na rangi ambazo ni kitambulisho cha vyama hivyo; Nyeusi, Manjano na kijani. Mzizi wa fitina ni mvutano unaoendelea kati ya walinzi wa mazingira die Grüne na chama kidogo cha kihafidhina CSU kuhusu kiwango cha juu cha wakimbizi wanaoruhusiwa kuingia humu nchini.

Mwenyekiti wa  chama cha walinzi wa mazingira, Bündnis 90, die Grüne, Simone Peter amesisitiza chama chake hakitoachia abadan kuwekwa kiwango kama hicho katika wakati ambako mwenyekiti mpya wa kundi la wabunge wa CSU wa jimbo la kusini la Bavaria katika bunge la shirikisho, Alexander Dobrindt anatilia mkazo madai hayo. Matamshi makali yametolewa leo nii na baadhi ya viongozi wa CDU dhidi ya msimamo wa mjini Munich. Waziri mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein Daniel Günther amesema CSU wanabidi wajiepushe na misimamo mikali ambayo inaweza kuhatarisha juhudi za kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne-unaojulikana kama muungano wa Jamaica. Daniel Günther binafsi anaongoza serikali ya muungano mjini Kiel ya vyama vya CDU,FDP na die Grüne.

Gavana wa Bavaria Horst Seehofer ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha CSUPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

"Katika serikali ya muungano pamoja nasi, paamoja apia na CDU na FDP hakutakuwa na kiwango cha juu cha wakimbizi" amesema mwenyekiti wa die Grüne Simone Peter katika mahojiano na gazeti la "Rheinische Post. "Hilo CSU wanabidi walizingatie kama kweli wanatilia maanani uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa jamaica." Dobrindt anasema lakini kwa upande wake kiwango cha juu cha idadi ya wakimbizi lazima kiwe sehemu ya makubaliano ya kuundwa serikali ya muungano. Kabla ya vyama ndugu vya CDU na CSU kuanzisha mazungumzo pamoja na FDP na die Grüne, wanabidi wenyewe kwanza wasiklilizane. "Tutaona kama kweli sisi ni ndugu" ameongeza kusema Dobrindt.

Mabango ya kisiasa; wa chama cha kijani Katrin Goering Özdemir Cem, wa FDP Christian Lindner na Angela Merkel wa CDUPicha: Imago/C. von der Laage

Mbali na die Grüne, waliberali wa FDP pia wanapinga kuwekwa kiwango cha juu cha wakimbizi wanaoruhusiwa kuingia humu nchini na wanapigania kuwepo sheria timamu kuhusu uhamiaji. Katika mahojiano na kituo cha matangazo cha Deutschlandfunk, waziri mkuu wa jimbo la Schleswig-Holstein, Daniel Günther amesema anasikitika kuona mazungumzo ya kubuni serikali ya muungano yanatuwama katika suala la kiwango cha juu cha wakimbizi.

Wakati huo huo kundi la wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU limependekeza waziri wa fedha Wolfgang Schäuble ateuliwe kuwa spika wa bunge la shirikisho Bundestag. Itafaa kusema hapa kwamba waliberali wa FDP,mojawapo ya wasjhirika katika serikali inayotarajiwa kuundwa ya muungano wa Jamaica wamesema tangu mwanzo wanataka wakabidhiwe wizara ya fedha pindi waakijiunga serikalini.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW