1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto zaongezeka wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu Congo

13 Desemba 2023

Zikiwa zimebaki siku chache kufanyika kwa uchaguzi nchini Congo, mzozo wa mashariki nchini humo na kucheleweshwa kwa vifaa vya uchaguzi ni miongoni mwa masuala yanayotia hofu kuelekea uchaguzi huo wa Desemba 20.

DRC | Wahlveranstaltung des Kandidaten und amtierenden Präsidenten Felix Tshisekedi
Picha: ARSENE MPIANA/AFP/Getty Images

Ikiwa imesalia wiki moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, bado kuna changamoto kadhaa za maandalizi ya uchaguzi huo, mzozo wa mashariki mwa nchi hiyo na kucheleweshwa kwa vifaa vya uchaguzi ni miongoni mwa masuala yanayotia hofu kuelekea uchaguzi huo wa Desemba 20.

Soma zaidi:Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza rasmi tarehe 20.11.2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 
Takriban wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha wanatazamiwa kupiga kura katika taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati Desemba 20, katika uchaguzi wa rais, wabunge, mikoa na manispaa.

Ukubwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unatajwa kuwa sawa na eneo la Ulaya Magharibi na hii inamaanisha kuwa kuandaa uchaguzi na kupata mpangilio sawa wa vifaa ni suala ngumu kufanikisha.

Uchaguzi nchini Congo unatarajiwa kufanyika Desemba 20.Picha: Stefan Kleinowitz/Zumapress/picture alliance

Nchi hiyo yenye takriban watu milioni 100 ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ikiwa na barabara chache ambazo tume huru ya uchaguzi CENI inataja kuwa ni mmojawapo ya kikwazo kikubwa katika kusambaza vifaa vya uchaguzi.

Soma zaidi: Wagombea 26 kuwania kiti cha urais Kongo

Takriban wagombea laki moja katika chaguzi zote nne wanashiriki, wakiwemo wagombea wa nafasi ya urais, huku Rais Felix Tshisekedi, ambaye aliingia madarakani baada ya uchaguzi uliogubikwa na utata mwaka 2018 akigombea tena uchaguzi huo kwa mara ya pili.

Licha ya wagombea wa urais wote wakuu na upinzani kuhimiza umakini kuelekea katika uchaguzi huo, lakini bado suala la udanganyifu linasalia kuwa jambo linalotiliwa shaka kabla ya upigaji huo wa kura wiki ijayo.

Upinzani nchini  Kongo  kwa muda mrefu umeishutumu serikali kwa kupanga tume ya uchaguzi pamoja na Mahakama ya Katiba ambayo ndiyo msuluhishi wa mwisho wa migogoro ya uchaguzi ingawa pamoja na hayo bado kuna wasiwasi kuhusu orodha halisi ya wapiga kura.

Denis Mukwege, mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais nchini CongoPicha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Martin Fayulu ambaye ni mwanasiasa wa upinzani amesema anaamini kuwa yapo majina ya uwongo milioni 10 kwenye orodha ya daftari la kura, huku akihamasisha wapiga kura kuwa makini na uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu huo.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchiniKongoAlain-Georges Shukrani ameliambia shirika la habari la AFP kuwa anadhani kuwa orodha hiyo haiaminiki na kwamba kuna imani ndogo sana katika mchakato wa uchaguzi. 

Upigaji wa kura nchini humo unatarajiwa kufanyika huku mzozo wa kivita ukiendelea katika eneo la mashariki ambalo limekuwa likikabiliwa na makundi yenye silaha kwa zaidi ya miongo mitatu sasa ambapo kundi la waasi wa M23 linalodaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda likiwa limeyateka maeneo mengi katika eneo hilo.