1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Changamoto zinazoukabili muhula mpya wa Kagame

18 Julai 2024

Wakati rais wa Rwanda Paul Kagame akijiandaa kuanza muhula wake wa nne madarakani, kiongozi huyo anakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohusiana na masuala ya ndani na pia ya kikanda.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Halil Sagirkaya/Anadolu/picture alliance

Baada ya Kagame kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu, wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kiongozi huyo anakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohusiana na masuala ya ndani na pia ya kikanda.

Miongoni mwa changamoto kuu zinamzomkabili rais Paul Kagame ambaye amekuwa akiiongoza Rwanda kwa mkono wa chuma tangu mwaka 2000, ni pamoja na kuendeleza ukuaji wa uchumi, kudumisha utulivu, kurekebisha mahusiano na jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na pia ikiwezekana hata kumteua mrithi wake.

Soma pia: Rais Kagame ashinda uchaguzi wa Rwanda kwa kishindo

Mahusiano kati ya serikali za Kigali na Kinshasa yamezorota tangu kuibuka tena mwishoni mwa mwaka 2021 kwa kundi la waasi la M23 mashariki mwa DRC. Kongo inalishutumu jeshi la Rwanda kwa kushirikiana na M23, madai ambayo pia yanaungwa mkono na ripoti za Umoja wa Mataifa ambazo zinaeleza kuwa wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanahusika moja kwa moja katika vita hivyo na kwamba Kigali ina "udhibiti kamili" wa operesheni za M23.

Kagame hajawahi kukanusha waziwazi uwepo wa majeshi yake nchini DRC, lakini akadhihirisha nia yake kwamba yuko tayari kuchukua hatua za kujihami ili kulinda maslahi ya taifa lake.

"Rwanda yategemea madini ya Kongo"

Rais wa Rwanda Paul Kagame (kushoto) akiwa na rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Paul-Simon Handy, Kiongozi anaeiwakilisha Taasisi ya Mafunzo ya Usalama barani Afrika amesema kuwa tafiti nyingi zinaonyesha kuwa mfumo wa maendeleo ya Rwanda unategemea pakubwa upatikanaji haramu wa maliasili hasa madini kutoka eneo la mashariki mwa Kongo.

Mtaalam huyo ameongeza kuwa hali hiyo ya utegemezi mbaya ndio unaosababisha migogoro na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa Rwanda kushirikiana na nchi nyingine kama DRC, Uganda na Burundi ili kuelekea kwenye mtindo wa kiuchumi ambao unahimiza ushirikiano kuliko vitendo vya unyonyaji.

Soma pia: UN: Wataalamu wasema wanajeshi kati ya 3,000 na 4,000 wa Rwanda walipelekwa nchini Kongo

Kwa upande wake, Ismael Buchana, mhadhiri wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Rwanda anasema mazungumzo ndiyo njia pekee ya kulifanikisha hilo, lakini akasisitiza kuwa hadi sasa, majaribio yote ya upatanishi hayajafaulu.

Kagame ambaye alichukua utawala huku uchumi wa Rwanda ukiwa katika hali mbaya, amejaribu kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kuboresha miundombinu ya taifa hilo. Licha ya yote hayo, uchumi wa Rwanda bado unategemea kwa kiasi kikubwa misaada ya kimataifa, ambayo imepungua katika muongo mmoja uliopita kutokana na ukosoaji juu ya ushiriki wake kwenye mzozo wa mashariki mwa DRC.

Umasikini bado ni tatizo kubwa Rwanda

Raia wa Rwanda wakiwa kwenye shughuli zao za kila siku mjini KigaliPicha: Luis Tato/AFP via Getty Images

Rwanda yenye rasilimali ndogo na isiyo na Bahari bado inakabiliwa na changamoto ya kuendelea kukuza uchumi wake. Licha ya mji wa Kigali kuonekana kuwa na majengo mengi ya ghorofa, umasikini miongoni mwa raia wa nchi hiyo bado ni tatizo kubwa.

Kulingana na Benki ya Dunia, takriban Mnyarwanda mmoja kati ya wawili ikiwa ni jumla ya asilimia 48.4 ya raia wote anaishi chini ya dola 2.15 kwa siku. Kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana, ambao ndio wengi kilifikia asilimia 16.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Louis Gitinywa, mwanasheria huko Rwanda na mchambuzi wa masuala ya siasa anasema kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, kupanda kwa mfumuko wa bei, elimu duni na umaskini, ni sawa na jipu ambalo ipo siku litatumbuka.

Mbali na suala hilo tete la kiuchumi na mahusiano na jirani yake DRC,  Kagame  amedai kuwa tangu mwaka 2010, amekuwa akikitaka chama chake kumtafuta mrithi wake, lakini kiongozi huyo aliidhinisha marekebisho yenye utata ya katiba ambayo licha ya kufupisha mihula ya urais kutoka miaka saba hadi mitano lakini yalimpa nafasi ya kusalia mdarakani hadi angalau mwaka 2034.

Suala la kumteua mrithi wa Kagame bado ni tete katika taifa hilo ambalo linaongozwa kwa mkono wa chuma na kiongozi huyo tangu kukomeshwa kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 800,000.

(Chanzo: AFP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW