1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanjo ya Covid 19 yawasili Kinshasa

3 Machi 2021

Awamu ya kwanza ya chanjo dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona iliwasili katika mji mkuu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Kinshasa, jioni ya Jumanne.

Ghana | AstraZeneca | COVAX-Impfstoff
Picha: Nipah Dennis/AFP

Hata hivyo, bado maoni ya raia wa Congo yanazidi kutofautiana kuhusu chanjo hiyo.

Dozi milioni moja nukta saba za chanjo hizo za Covid-19 zimefikishwa mjini Kinshasa jana kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ndjili. Sherehe rasmi ya mapokezi iliandaliwa mbele ya waziri wa afya ya umma Eteni Longondo na mwenzake wa mawasiliano na vyombo vya habari akiwa pia msemaji wa serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Jolino Makelele.

Wakati wa semina iliyoandaliwa na mpango wa chanjo ulioangazia mikakati ya mawasiliano ya kuanzishwa kwa chanjo dhidi ya janga hili, kiongozi wa mpango huo Elisabeth Munkamba alibainisha kwamba kampeni ya kwanza ya chanjo itawalenga wafanyikazi wa afya, wazee na wale wanaoweka hatari kubwa haswa kuhusu magonjwa ya Covid- 19, shinikizo la damu, na kisukari. Elisabeth Munkamba anaelezea.

Congo itapokea karibu dozi milioni sita za chanjo ya Astrazeneca

"Changamoto kwa sasa ni kujua mahali pa kufanyia chanjo, jinsi matangazo yatasambazwa ili watu waelewe vizuri, kutambua pia kipaumbele kwa sababu sio kila mtu atafaidika na chanjo hii kwanza, sio chanjo ya kulazimishwa, lakini kwa wazee walio katika hatari ya kukuza hali kali ya magonjwa hadi kufa kutokana na ugonjwa huo, wahudumu wa afya ambao wanaishi na wagonjwa kila siku na kadhalika, wanahusika. Lazima basi tufafanue vizuri jinsi tutakavyowapa chanjo watu hawa,” alisema Munkamba.

Jumla ya dozi milioni sita za chanjo iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Astra Zeneca / Oxford imepangwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi hii ikiwa kwenye orodha ya nchi za kwanza kupokea dozi hizi za chanjo zilizoidhinishwa haraka na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Familia zinavyopambana na COVID-19 Bukavu, DRC

02:01

This browser does not support the video element.

Hii itawezekana kupitia COVAX, mpango wa ulimwengu wa kuhakikisha upatikanaji wa haraka na usawa wa chanjo za COVID-19 kwa nchi zote, bila kujali kiwango cha mapato yao.

Maambukizi ya virusi vya corona Congo sasa ni 26 elfu

Lakini hadi sasa, baadhi ya raia wa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wameingiwa na hofu kutokana na chanjo hiyo. Tangu wiki moja, baadhi ya wazazi wamezuru shule na kuondoa watoto wao kutokana na fununu mbaya zilizosambazwa katika miji ya Bukavu, Rutshuru, Kinshasa, Kamanyola na Lubumbashi.

Lumière Singay ni mtaalamu wa masuala ya afya. Anaonya raia wa Congo kutulia na kuepuka habari mbaya za kuwatia hofu kuhusu chanjo hiyo.

Tangu kutangazwa janga la corona nchini Congo mwaka mmoja uliopita, nchi hii imefikia idadi ya wagonjwa elfu 26 na vifo zaidi ya mia saba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW