Chanjo ya majaribio ya virusi vya Corona yazusha mjadala DRC
8 Aprili 2020Mjadala mkali umeibuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya serikali kukubali majaribio ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. Raia wengi mjini Kinshasa walitupilia mbali pendekezo hilo na kuitaka serikali kurejelea hatua hiyo. Wakati huo huo maoni mengi yameibuka kwenye nchi zinazozungumza kifaransa, ili kukosoa vikali matamshi ya watafiti wawili wa Ufaransa ambao walipendekeza kuanzisha utafiti wa majaribio ya chanjo barani Afrika.
Hatua ya serikali ya kuridhia kuendeshwa utafiti wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona nchini Congo imezua mjadala mkali. Kwenye mitandao ya kijamii raia wengi wametupilia mbali majaribio ya nchanjo hiyo kuendeshwa nchini. Hiyo ni kufuatia matamshi ya kiongozi wa kamati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa wa Corona, Jean-jacques Muyembe kuelezea kwamba Congo ni miongoni mwa nchi zilizochaguliwa ili kuanzisha majaribio ya chanjo dhidi ya Corona.
Kwenye barua yao ya wazi kwa daktari Muyembe, mashirika ya kiraia yameelezea kwamba hakuwezi kuweko na nchanjo ya majaribio pasina na mjadala wa kitaifa ili kuwashawishi raia. Bienvenu Matumo, mwanachama wa kundi la vijana kwa ajili ya mageuzi, LUCHA amesemakwamba chanjo ya majiribionilazima ianzie Ulaya ao kwenye nchi zilizoathirika zaidi.
''Tumewatahadharisha viongozi wetu kwamba sisi vijana wa Afrika hatuwezi kukubali chanjo hiyo ya majaribio kuanzia barani humu.Ikiwa itanzishwa basi ianziye huko ambako ugonjwa umeripuka na kwenye nchi zilizoathirika''.
Afrika siyo mahabara ya utafiti wa kisayansi
Kufuatia shinikizo kutoka kwa wananchi, Dr Muyembe alirejelea matamshi yake na kusema hakutokuweko majaribio yoyote ya chanjo hadi hapo shirika la afya ulimwenguni litakapoidhinisha chanjo hiyo.
Omar Kavota, kiongozi wa shirika la haki za binadamu nchini Congo, CEPADHO ameonya kuwa serikali inatakiwa kuwahamasisha vyema wananchi kuhusu vita dhidi ya Corona, ili kuepuka raia kupoteza imani na viongozi kwa kipindi hiki kigumu.
''Kitu ambacho hatutakubaliana nacho ni ikiwa chanjo hiyo itashurutishwa kwa raia wote,na hapo itakuwa ni ukeukaji wa haki za binadamu, lakini ikiwa itakuwa kwa ihari ya kila mtu basi hakuna cha kujuta kwa sababu niya ni kuwakinga raia wa Congo''.
Mjadala huo unafuatia pia matamshi ya watafiti wawili wa Ufaransa ambao walielezea kwamba kabla ya kutumiwa nchini Ufaransa, chanjo hiyo ya majaribio inatakiwa kufanyiwa majaribio huko barani Afrika.
Mkuu wa shirika la Afya ulimwenguni, Tedros Gebreyesus aliyataja matamshi hayo kuwa ya kibaguzi na ya kikoloni. Gebreyesus aliendelea kusema kuwa, urithi ya tabia ya ukoloni unatakiwa kukomeshwa.
Mchezaji kandanda wa zamani kutoka Ivory Coast,Didier Drogba aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba, Afrika siyo mahabara ya kuendesha utafiti wa kisayansi.
Shirikisho la mawakili wa Morocco linaelezea kwamba litawashitaki madaktari hao wa Ufaransa. Kwa upande wake msemaji wa rais wa Senegal, Macky sall, ameelezea kwamba matamshi hayo ya watafiti wa Ufaransa ni upuuzi wa kikoloni.
Kwenye taarifa yake, wizara ya mammbo ya nje ya Ufaransa inaelezea kwamba matamshi hayo siyo msimamo wa viongozi wa serikali yake.