1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanjo ya Malaria kuanza kutumika Ghana

13 Aprili 2023

Chanjo ya Malaria iliyotengenezwa na chuo kikuu cha Uingereza cha Oxford inatarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni nchini Ghana. Hii ni Mara ya kwanza chanzo hii kuidhinishwa kutumika duniani.

Symbolbild Malaria | Spritze
Picha: Brian Ongoro/AFP

Kulingana na taarifa ya chuo kikuu cha Oxford, chanjo hiyo imeidhinishwa kutumika kwa watoto walio na umri wa miezi mitano hadi 36. Watoto wengi walio ndani ya umri huo ndio wanaokuwa hatarini kufa kutokana na ugonjwa wa Malaria. Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa inatumai chanjo hii muhimu ya mwanzo, itawasaidia raia wa Ghana na watoto wa Afrika kuudhibiti ugonjwa wa Malaria.

Profesa Adrian Hill, mchunguzi mkuu wa mpango wa chanjo ya R21/Matrix-M na pia mkurugenzi wa taasisi ya Jenner katika chuo kikuu cha Oxford, amesema utafiti wa takriban miaka 30 wa chanjo ya Malaria katika chuo hicho umepelekea kupatikana kwa chanjo hii mpya iliyo na ufanisi mkubwa inayoweza kusambazwa kwa nchi zilizo na uhitaji zaidi.

BioNTech kufanya majaribio chanjo ya Malaria

Mwezi Septemba mwaka jana, chuo kikuu cha Oxford kilisema aina mpya ya chanjo ya Malaria imeendelea kuonesha kiwango kikubwa cha kinga dhidi ya ugonjwa huo, na kutoa maoni kwamba chanjo hiyo ambayo bei yake ni nafuu inaeza kuanza kutengenezwa kwa wingi katika miaka ijayo.

Chanjo ya Oxford yaripotiwa kuwa na nguvu kuliko chanjo ya GSK

Picha: DW

Nalo kundi la watafiti wa kimataifa lilipendekeza kwamba chanjo hiyo inaweza kuleta mabadiliko katika juhudi zilizowekwa kupambana na ugonjwa wa Malaria ambao mwaka 2020 pekee, ulisababisha vifo vya watu 627,000 wengi wao watoto kutoka bara la afrika.  

WHO yataka fedha za mapambano ya malaria ziongezwe

Mwaka uliopita chanjo nyengine tofauti iliyotengenezwa na kampuni ya madawa ya Uingereza ya GlaxoSmithKline (GSK) ilikuwa ya kwanza kuidhinishwa na shirika la afya ulimwenguni WHO, kutumika kwa wingi dhidi ya ugonjwa huo. Kwa sasa chanjo hiyo imeshatolewa kwa zaidi ya watoto milioni moja barani Afrika.

Licha ya hayo utafiti umegundua kuwa ufanisi wa chanjo ya GSK- unafikia kiwango cha asilimia 60 na makali yake yanapungua hata baada ya kudungwa chanjo nyengine ya ziada au dozi ya pili ya chanjo hiyo.

Hata hivyo chanjo ya chuo kikuu cha Oxford ya R21/Matrix-M imegundulika kuwa na ufanisi wa  asilimia 77 ya kinga dhidi ya Malaria, hii ikiwa ni kulingana na utafiti uliofanywa mwaka uliopita. Hii inaashirika kwamba lengo la WHO la kupata chanjo inayofikia kinga kwa asilimia 75 limetimia.

Chanzo: afp