Chanjo ya virusi vya Ukimwi kwa mataifa ya Afrika
16 Oktoba 2025
Hata hivyo, huku matabibu wakipongeza chanjo hii ya ‘miujiza', wenyeji wana mashaka mbalimbali kuihusu ikiwemo bei yake na pia madhara yanayoweza kutoka na sindano hiyo atakayodungwa mtu mara mbili kwa mwaka.
Chanjo ya sindano dhidi ya virusi vya UKIMWI Lenacapavir kwa ufupi LEN inayotolewa mara mbili kwa mwaka kwa mtu imepangwa kutolewa Zimbabwe, nchi hiyo ikiwa miongoni mwa mataifa kumi yaliyoorodheshwa kwa ajili ya mpango huo unaoanza mwaka 2026.
Chanjo kutolewa katika mataifa ya Afrika Mashariki pia
Mataifa mengine ni Kenya, Nigeria, Zambia, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Eswatini na Botswana.
Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe umelezea furaha yake kwamba Zimbawe imo katika kundi la mataifa hayo. Itakumbukwa kuwa asili mia 4 ya watu walio na virusi duniani wamo katika nchi hiyo, huku takwimu za maambukizi zikiwa watu milioni 1.3 kwa mujibu wa mwaka 2024.
Lakini pia Zimbabwe imepata mafanikio kadhaa katika kupambana na virusi vya UKIMWI. Mojawapo ya mafanikio hayo ni kutimiza azma shirika la Umoja Mataifa linaloshughulikia masuala ya UKIMWI UNAIDS.
Wataalamu wanaamini kuwa kuzinduliwa kwa chanjo ya Lenacapavir kutachangia zaidi katika juhudi za nchi hiyo za kumaliza maambukizi.
Zoezi hilo nchini Zimbabwe linatarajiwa kuwalenga watu waliomo katika hatari ya kuambukizwa wakiwemo wasichana mabarobaro pamoja na akina mama wajawazito na wale ambao wananyonyesha.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, chanjo hii ni hatua bora zaidi katika ufumbuzi wa kuepusha maambukizo ya UKIMWI. Hii pia ni njia muafaka kuwawezesha watu kama makahaba walio katika hatari kubwa kuambukizwa UKIMWI.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alinukuliwa akisema " Huku chanjo dhidi ya Virusi vya UKIMWI ikiwa bado inatafutwa, chanjo hii ya Lenacapavir ni mafanikio makubwa. Hii ni kutokana na matokeo ya majaribio mbalimbali yaliyofanywa na kuweza kuepusha maambukizi miongoni mwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa.”
Kwa upande wake Naibu mkurugenzi wa UNAIDS Angei Achrekar aliambia DW kwamba
"Tunaizungumzia chanjo hii ya miujiza. Kwa sasa ukweli ni kwamba chanjo hiyo ina takriban asili mia moja katika kuepusha maambukizi mapya, haikutarajiwa. Ni ufumbuzi bora zaidi katika kupambana na UKIMWI," alisema Angei.
Chanjo hii ya Lenacapavir inatarajiwa kuanza kutolewa katika mataifa 120 kufikia mwaka 2027 na inatarajiwa kupunguza maambukizo mapya yapatayo milioni 1.3 kila mwaka.
Ikilinganishwa na chanjo za mwezi au siku, Lenacapavir itatolewa mara mbili kwa mwaka. Mtaalaamu wa afya nchini Zimbabwe Daktari Ponesai Nyika ameiambia DW kwamba chanjo hiyo inafanya vyema ikiwa itatumiwa ipasavyo.
Chanjo hiyo imefanyiwa majaribio mara mbili. Moja miongoni mwa wanawake na wasichana Kusini mwa jangwa la Sahara na kwingineko miongoni mwa watu wa mapenzi ya jinsia moja nchini Marekani.
Raia wa Zimbabwe wafurahia chanjo
Katika majaribio hayo mawili, chanjo hiyo ilikuwa na matokeo ya asili mia 99 na kwa hiyo kudhihirisha kuwa inaweza kuepusha maambukizo ya virusi ikiwa itatolewa.Kwa kuwa dawa hiyo hutolewa mara mbili kwa mwaka, daktari Nyika anafafanua zaidi kwamba hii inapunguza visa vya watu kutohudhuria matibabu.
Huku raia wa Zimbabwe wakifurahia habari za chanjo hii, wengine wana mashaka kuihusu. Daktari Nyika anaondoa dhana kwamba kama dawa zingine zilizo na madhara na amewataka wataalamu katika mataifa ya Afrika kuitumia kwa njia ya uwazi na kuelimisha ipasavyo kuhusu madhara yake.
Lakini kwa wengine kero yao ni bei ya chanjo hiyo. Raia mmoja wa Uganda aliyeongea na DW alihoji uwezekano wa kukidhi bei ya dola 40 kila mwaka akisema kuwa chanjo hiyo ni ya watu matajiri.Awali chanjo hiyo iligharimu dola elfu 28 kila mwaka. Ni kwa ajili hii ndipo baadhi ya watu wanapendekeza chanjo hiyo itengenezwe katika mataifa ya Afrika ili kupunguza bei yake.
Ili kuondoa mashaka kuhusiana na bei, ifahamike kuwa shirika la mpango wa rais wa Marekani katika kutoa misaada ya kwa ajili ya virusi vya UKIMWI (PEPFAR) na lile la Global Fund watafanya mpango wa kuona kwamba bei hiyo inapunguzwa.