Chanzo cha ajali ya ndege bado hakijajulikana Tanzania
9 Novemba 2022Akizungumza katika mkutano na waandishi habari uliofanyika leo jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, TCAA Hamza Johari, amesema uchunguzi wa awali kuhusu chanzo cha ajali hiyo utatolewa baada ya siku 14.
Ingawa alisoma taarifa ya awali kuhusu ajali hiyo iliyotolewa na kitengo cha uchunguzi wa ndege kilicho chini ya wizara ya ujenzi na miundombinu.
Chanzo cha ajali Tanzania bado kitendawili.
Akisoma taarifa ya awali ya uchunguzi wa ajali hiyo ambayo imeonyesha aina ya ndege, rubani, mwelekeo wa safari, idadi ya abiria waliofariki, waliokolewa, Johari amesema sababu ya ajali hiyo bado haijulikani. Uchunguzi wa awali ulianza siku ile ile ajali ilipotokea.
Amesema Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga na imesaini mkataba wa Chicago wa mwaka 1942, na hivyo ili kutoa taarifa inabidi wafuate taratibu za kimataifa na kisheria.
Kadhalika amewataka Watanzania waache kupotosha kuhusu usalama wa viwanja vya ndege nchini na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo si uwanja wa ndege wa Bukoba, kwani uwanja huo ni mkongwe.
Ukaguzi wa mpya wa ndege zote nchini Tanzania
Kadhalika mamlaka hiyo imesema inafanya ukaguzi wa viwanja vya ndege katika viwanja na kuhakikisha ubora wa ndege zote nchini kuhakikisha vina ubora wa kutoa usafiri wa anga, kutoka kituo kimoja kwenda kingine.
Wakati huo huo, Shirika la Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH) limepoteza watumishi wake watano kati ya wanane waliokuwa katika ndege hiyo, siku ya Jumapili. Watumishi hao waliagwa jana katika viwanja vya Karimjee huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Dk. David Sando akisema walikuwa wanaelekea Tabora kufanya tathmini ya mwaka ya miradi ya shirika hilo.
Soma zaidi:Tanzania kuaga miili ya waliofariki katika ajali ya ndege
Taasisi nyingine zilizopoteza nguvu kazi ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA).