Chavez apata maambukizi mapya
5 Machi 2013Rais huyo wa Venezuela ambaye wakati mmmoja alikuwa ndiye nguzo kuu ya Amerika kusini sasa amesalia kutumia mirija ili kumsaidia kupumua. Chavez hajaonekana wala kuzungumza hadharani kwa karibu miezi mitatu sasa na hivyo basi kuliacha taifa lake lililo na utajiri mkubwa wa mafuta na kanda hiyo ya Amerika kusini kwa jumla kataika hali ya ati ati.
Waziri wa Habari wa Venezuela Ernesto Villlegas amesema kwenye taarifa iliyosomwa kutoka hospitali alikolazwa rais huyo kuwa Chavez amekumbwa na maambukizi mapya na makali zaidi ambayo yametatiza kupumua kwake.
Taarifa hiyo inawadia wiki mbili baada ya Chavez aliye na umri wa miaka 58 kulazwa katika hospitali ya kijeshi ya Caracas punde tu baada ya kutoka kupokea matibabu nchini Cuba kwa miezi miwiwli alipofanyiwa upasuaji wa nne wa kudhibiti sarartani tangu mwezi Juni mwaka 2011.
Upinzani watilia shaka hali ya Chavez
Kutokuwepo kwa Chavez katika kuendesha serikali ambapo hata hakuweza kuapishwa kwa hatamu yake ya tatu madarakani ya kipindi cha miaka sita ijayo kumeughadhabisha upande wa upinzani ambao unaishutumu serikali kwa kudanganya kuhusu hali yake ya kiafya.
Mamia ya watu wakiongozwa na upande wa upinzani walijitokeza Jumapili iliyopita kuandamana kutaka kujua ukweli wa mambo kuhusu hali halisi ya rais huyo mwenye ushawishi mkubwa katika kanda hiyo ya Amerika kusini.
Maafisa wa serikali wametoa picha chache tu zikimuonyesha Chavez akiwa amelala kitandani mwake huko Havana akiwa na mabinti wake wawili mnamo tarehe 15 mwezi Februari siku tatu kabla alipokuwa akitarajiwa kurejea nyumbani. Kutokuonekana kwake kwa umma na kimya cha serikali kumezua uvumi kuhusu afya yake.
Makamu wa Rais Nicolas Maduro na maafisa wengine wakuu wa serikali ya Venezuela wamewakashifu vikali upinzani kuhusiana na madai kuwa Chavez huenda amefariki ama yuko karibu kufariki wakisema ni njama ya kuyumbisha taifa hilo.
Raia watakiwa wawe watulivu
Waziri wa Habari Villegas amewataka raia wa taifa hilo kusimama kidete dhidi ya kile alichokitaja vita kutoka nje ya taifa hilo na mafisadi walioko Venezuela ambao wamemtusi,kumkejeli na kumchukia rais wao ambao sasa wanatumia hali yake ya kiafya kujaribu kuleta machafuko.
Maduro anayeonekana kuwa mrithi wa Chavez amekuwa akitoa taarifa zinazokinzana kuhusu uwezo wa rais huyo kuendesha majukumu yake akiwa hospitalini. Chvez ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 14 sasa,alishindwa kuhudhuria shughuli ya kuapishwa kwake tarehe 10 mwezi Januari na mahakama ya juu nchini humo ikahirisha shughuli hiyo kwa muda usiojulikana
Kabla ya kuelekea Cuba mwezi Desemba, Chavez alimteua Maduro kama mrithi wake kisiasa na kuwahimiza raia wa Venezuela kumchagua iwapo atashindwa kurejelea majukumu yake. Katiba ya taifa hilo inasema kuwa uchaguzi unapaswa kuitishwa katika kipindi cha siku thelathini endapo rais atashindwa kutekeleza majukumu yake.
Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman