Chen Guancheng azungumza na bunge la Marekani
4 Mei 2012Yalikuwa mazungumzo yasiyo ya kawaida. Kwa dakika kadhaa wabunge wa Marekani walikuwa wameunganishwa kwa njia ya simu na Chen Guancheng aliyekuwa akizungumza kutoka hospitalini. Mazungumzo ya simu yaliwekwa kwa sauti ya juu ili kuwawezesha wabunge wote kuyasikia. Mkalimani alikuwepo kuyatafsiri maneno ya Chen.
"Ninataka kukutana na waziri Clinton". Hayo ndiyo yalikuwa matakwa ya mwanaharakati huyo kwa bunge la Marekani lililokuwa limekutana kujadili kuhusu China. Chen alieleza kwamba anatarajia kupata msaada kutoka kwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani. Alitaka pia kumshukuru waziri huyo ambaye hadi leo asubuhi alikuwa ziarani China.
Chen aliendelea kusema kwamba anataka kukutana na Hillary Clinton kwa sababu yeye, mke na watoto wake wanataka kuondoka China wakisafiri katika ndege ya waziri huyo. Mkalimani wa Chen, Bw. Bob Fu, ni rafiki wa karibu wa mwanaharakati huyo na vile vile ni mwenyeketi wa shirika la kutetea haki za binadamu liitwalo ChinaAid, lenye makao yake makuu Texas, Marekani. Fu alilieleza bunge la Marekani kwamba kwa mujibu wa Chen, haya ndiyo aliyoambiwa alipokuwa amekimbilia katika ubalozi wa Marekani mjini Beijing: "Wamarekani walimwambia kwamba asipoondoka katika ubalozi wao mara moja, basi hutokuwa na nafasi ya kumwona tena mke wake na watoto wake."
Chen aruhusiwa kwenda kusoma katika nchi za nje
Shirika la ChinaAid pamoja na mwenyekiti wake Fu, wanaushutumu ubalozi wa Marekani kwa kumhamasisha Chen aondoke katika ubalozi huo haraka mno. Fu ameeleza kwamba lilikuwa kosa kumshawishi Chen aondoke baada ya siku sita tu badala ya kumpa muda zaidi. Chen aliliambia gazeti la kwenye mtandao la Daily Beast kwamba jambo analotamani zaidi kwa wakati huu ni kupata nafasi ya kusafiri kwenda Marekani pamoja na familia yake, mapema iwezekanavyo.
Leo asubuhi, wizara ya mambo ya kigeni ya China imetangaza kwamba Chen anaruhusiwa kwenda kusoma katika nchi za nje. Tamko hilo linaashiria kwamba huenda mwisho wa mgogogro wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Marekani umekaribia.
Mwandishi: Ralf Sina/Elizabeth Shoo
Mhariri: Othman Miraji