1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChile

Chile yafanya kura nyingine ya maoni kubadili katiba

17 Desemba 2023

Raia wa Chile wanapiga kura kwa mara nyingine leo kuamua juu ya rasimu ya katiba inayolenga kuchukua nafasi ya ile iliyotungwa enzi ya utawala wa kidikteta wa Augusto Pinochet.

Upigaji kura ukiendelea Chile
Upigaji kura ukiendelea ChilePicha: SEBASTIAN CISTERNAS/Aton Chile/IMAGO

Kura hiyo ya leo ni ya pili katika kipindi cha miaka minne iliyopita ikiwa ni juhudi za taifa hilo kubadili katiba iliyopo baada ya shinikizo kutokana na maandamano makubwa yaliyoitikisa Chile mwaka 2019.

Rasimu ya kwanza iliyojumuisha kwa sehemu kubwa misingi ya kiliberali ikiwemo usawa ndani ya jamii na haki za jinsia ilikataliwa na wapigakura mnamo Septemba mwaka jana.

Rasimu inayopigiwa kura hii leo inazingatiwa kuwa ya kihafidhana zaidi kuliko katiba ya sasa iliyoandikwa mwaka 1980 na utafiti wa maoni ya umma unaonesha  huenda itakataliwa pia na wapigakura.