1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China haina nia ya kupigana vikumbo na wengine-Xi Jinping

18 Desemba 2018

China yaadhimisha miaka 40 tangu ilipoanzisha mageuzi ya kiuchumi na kufungua milango ya kibioashara kwa kusisitiza kwamba inafahamu vitisho itakavyokumbana navyo katika juhudi zake za kusaka zaidi maendeleo yake

China Rede Xi Jinping 40. Jahrestag Reform und Öffnung
Picha: Reuters/J. Lee

Rais wa China Xi Jinping ametowa hotuba iliyotowa sura ya kuionesha China kama mojawapo ya nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani. Katika maadhimisho ya miaka 40 ya mageuzi na kufunguwa milango ya maendeleo ya  chama cha kikomunisti XI amesema China haitojijenga kwa gharama ya maslahi ya nchi nyingine.

Hotuba ya rais wa China Xi Jinping ya miaka 40 ya mageuzi ya kiuchumi kiongozi huyo amerudia kwa mara nyingine kubaini ilivyojitolea nchi hiyo katika kuwa na mfumo wa kimataifa wa kibiashara na kufungua zaidi uchumi wake, ingawa pia hakutangaza juhudi nyingine zozote mpya za kupambana na hali ya ukuaji taratibu wa uchumi pamoja na misuguano ya kibiashara iliyopo kati yake na Marekani. Badala yake kiongozi huyo wa kikomunisti ameonekana kuuangalia zaidi mustakabali wa nchi hiyo.

"Kila hatua katika mfumo wetu wa mageuzi na kufungua milango sio rahisi. Huko baadaye tunaweza kukabiliwa na hatari kila aina pamoja na changamoto na hata vimbunga vya mitikisiko isiyoweza kufikirika."

Picha: Reuters/C. Jasso

China inajitanua duniani kote kuanzia Asia,nchi zilizoko kwenye eneo la bahari ya Pacific mpaka barani Afrika kupitia mtandao wa miradi mbali mbali ya miundo mbinu ikijihusisha hasa na ujenzi wa barabara na reli na haya ni mambo ambayo yamesababisha baadhi ya nchi kuanza kuwa na wasiwasi kuhusu kile ambacho wanakitaja kama ni kutanuka kwa ushawishi wa China. China inakosolewa katika ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi.

Wakati rais Xi akisema kwamba China inajiimarisha zaidi kuelekea kwenye nafasi ya juu kabisa ya jukwaa la dunia pia amebaini kwamba nchi hiyo inataka kutafuta sera ya kutetea ulinzi wa kitaifa.

Lakini pia anasisitiza kwamba maendeleo ya China sio kitisho kwa nchi yoyote ile, kwa sababu kwa mtazamo wa kiongozi huyo ni kwamba haijalishi ni kwa kiasi gani China inapiga hatua,haitowahi hata siku moja kutaka kuwa na mamlaka juu ya nchi nyingine.

Picha: Reuters/K. Lamarque

Katika maadhimisho hayo watu 100 walitambuliwa kama waanzilishi wa mageuzi ya kiuchumi ya China akiwemo kiongozi wa zamani Deng Xiaoping aliyepewa heshima maalum na rais Xi. Deng ametajwa kwamba ni kiongozi aliyeinusuru China kutoporomoka kiuchumi kufuatia mapinduzi wa kijadi.Ni mtu aliyeanzisha mageuzi ya kuleta soko huru China.Miaka ya nyuma sherehe za kumbukumbu ya mageuzi ya China zilikosolewa na wasomi kwa kupuuzwa dhima aliyokuwa nayo Deng katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini humo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/Coonan Clifford

Mhariri:Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW